Feb 08, 2020 02:57 UTC
  • Ripoti: Makumi waliuawa mwaka jana katika hujuma za al-Shabaab Kenya

Uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya Haki za Binadamu na Sera umebainisha kuwa, watu wasiopungua 83 waliuawa nchini Kenya mwaka uliopita wa 2019 katika mashambulizi ya kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab lenye makao makuu yake katika nchi jirani ya Somalia.

Kwa mujibu wa ripoti ya uchunguzi huo, maafisa usalama 42 na raia 26 ni miongoni mwa Wakenya waliouawa katika hujuma za kigaidi za al-Shabaab nchini humo mwaka jana 2019.

Idadi hiyo inaonyesha kuwa, kulikuwa na ongezeko la asilimia 20 ya mauaji yaliyofanywa na wanachama wa al-Shabaab nchini Kenya mwaka jana, kwani mwaka juzi 2018, idadi ya watu waliouawa na genge hilo la ukufurishaji ilikuwa 56.

Katikati ya Januari 2019, raia 21 waliuawa katika shambulio la kigaidi ambalo genge la kitakfiri la al-Shabaab la nchini Somalia lilitangaza kuhusika nalo, dhidi ya Hoteli ya Dusit D2 jijini Nairobi.

Ramani ya Kenya na jirani zake

Kaunti za Wajir, Mandera na Garissa za kaskazini mashariki na hata kaunti ya Lamu pwani ya Kenya zimekuwa zikilengwa na al-Shabaab katika mashambulizi yake ya mara kwa mara.

Mapema mwaka huu, walimu wanne waliuawa katika shambulizi la kuvizia la al-Shabaab katika Kaunti ya Garissa, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Kundi hilo la kigaidi ambalo ni tawi la mtandao wa kigaidi al-Qaeda nchini Somalia limefanya mashambulizi mengi ya kigaidi katika nchi jirani ya Kenya likilenga idara za serikali, askari, magari ya abiria na mahoteli, tangu Kenya itume wanajeshi wake (KDF) katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Tags

Maoni