Feb 12, 2020 12:50 UTC

Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki amesema wanafunzi wanaosoma katika mji wa Wuhan hawawezi kurudi kwa sababu kuna katazo la kutoingia wala kutoka kwenye mji huo kutokana na maambukizi ya virusi vya corona.

Hatua hiyo inafuatia baada ya wanafunzi wanaosoma katika mji huo kuiomba serikali iwasaidie warudi nchini kutokana na kasi ya ongezeko la vifo na maambukizi ya virusi hivyo.

Juzi pekee watu 103 walifariki dunia kutokana na virusi hivyo na kufanya waliofariki dunia hadi sasa kufikia 1,016 lakini maambukizi mapya yameshuka kwa asilimia 20 kutoka watu 3,062 hadi 2,478.

Balozi Kairuki akizungumzia suala la wanafunzi hao, alisema katazo la watu kutembea limesababisha msongo wa mawazo kwa watu wengi wakiwemo wanafunzi hao na kusisitiza lazima wafuate masharti ya usalama.

Balozi Kairuki alisema hivi na hapa ninamnukuu, “nimeiona video ya vijana wetu wakitaka waondolewe. Ugonjwa upo katika nchi nzima ya China, lakini umeenea zaidi jimbo la Hubei, hasa mji wa Wuhan ambako wako vijana hao. “Ukifungiwa muda mrefu lazima utakuwa na ‘stress au depression’ na hali hii ndiyo inayopelekea vijana wetu watake waondolewe.

Wanafunzi wa Tanzania katika mji wa Wuhan wakitoa wito wa kurejeshwa nyumbani 

“’Weekend’ nilikuwa na kikao na viongozi wao kwa sababu siruhusiwi kwenda huko na hata hapa Beijing siruhusiwi hata kusogea nje ya geti,” alisema Balozi Kairuki.

Alisema hakuna mtu anayeruhusiwa kuingia au kutoka nje ya jimbo au mji huo na kila aliyeko ndani anatakiwa kuchukua tahadhari kwa kukaa ndani ya nyumba, kuepuka misongamano na kuzingatia kanuni za usafi.

Katika video iliyosambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, Watanzania wanaosoma Wuhan wameonekana wakiwa na mabango yaliyosomeka ‘Please, please, please’, ‘Dear Tanzania please bring us home, ‘We are not infected yet’.

Tags

Maoni