Feb 15, 2020 13:53 UTC
  • Haftar akataa kutekeleza azimio la UN la wito wa kusitisha vita nchini Libya

Kamanda wa kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya (LNA) amekataa kutekeleza azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalozitaka pande zinazopigana nchini Libya kusitisha vita.

Jenerali Khalifa Haftar, kamanda wa vikosi vya kundi la LNA amekataa kutekeleza azimio la usitishaji vita lililopitishwa na Baraza la Usalama la UN na kusisitiza kuwa, kundi lake litaendeleza vita dhidi ya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa (GNA).

Haftar amesema, vikosi vyake havitarudi nyuma wala havitafanya mapatano yoyote mpaka viuteke mji mkuu Tripoli.

Akijibu kauli hiyo ya Haftar, Muhammad Ammari Zaed, mjumbe  wa baraza la uongozi la Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya amesema, matamshi ya Khalifa Haftar yanadhihirisha mbinu anayotumia ya kuvuta muda wa kuvikusanya pamoja vikosi vyake na kujizatiti upya kwa zana na silaha zaidi ili kufanya shambulio tena dhidi ya Tripoli.

Ammari Zaed ameongeza kuwa, hatua ya Haftar mtenda jinai ya kung'ang'ania kuendeleza mapigano na vita dhidi ya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya inabainisha nafasi ya nchi zinazomhami na kumuunga mkono katika kuvuruga jitihada za kimataifa na kukataa kutekeleza maazimio ya kimataifa ya usitishaji vita.

Kikao cha Baraza la Usalama la UN

Mjumbe huyo wa Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya amebainisha kuwa, kwa kuwepo Haftar, haitapatikana njia yoyote ya utatuzi wa kisiasa nchini Libya.

Siku ya Jumatano ya tarehe 12 Februari, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha rasimu ya azimio la usitishaji vita nchini Libya kulingana na matokeo ya mkutano wa Berlin.

Itakumbukwa kuwa mnamo mwezi Aprili, 2019, vikosi vya Khalifa Haftar vinavyoungwa mkono na Imarati, Saudi Arabia na Misri pamoja na baadhi ya nchi za Ulaya vilianzisha hujuma na mashambulio dhidi ya Tripoli kwa lengo la kuuteka mji mkuu huo wa Libya unaodhibitiwa na Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya nchi hiyo inayotambuliwa rasmi kimataifa.../ 

Tags

Maoni