Feb 16, 2020 02:51 UTC
  • Vijana wa Sudan wasimulia jinsi Abu Dhabi ilivyowapeleka kupigana vita Libya

Vijana wa Kisudan waliorejea makwao hivi karibuni wamesimulia jinsi walivyohadaiwa na kampuni ya Black Shield Security Services iliyowaahaidi kuwapa kazi za ulinzi na badala yake walijikuta wakipewa mafunzo ya kijeshi yasiyooana na kazi zao na kupelekwa bila ya kujua huko Libya na Yemen kupigana vita.

Baadhi ya vijana hao wa Kisudan waliorejea nchini kwao wiki mbili zilizopita wamesema kuwa, walipelekwa wakiwa 270 katika eneo la Hilali ya Mafuta nchini Libya bila ya wao wenyewe kujua na bila ya kuwa na viza. Wanasema awali walisafirishwa hadi Imarati ambako walipewa mafunzo ya kijeshi kisha wakasafirishwa kwa ndege ya kijeshi na kujikuta wakiwa Libya baada ya safari ya masaa mengi.

Mwishino mwa mwezi Disemba mwaka jana taasisi moja ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu ililaani vikali hatua ya Umoja wa Falme wa Kiarabu (Imarati) ya kuwaajiri mamluki wa Kisudani wanaotumiwa kupigana bega kwa beba na mbabe wa kivita wa Libya, Jenerali Khalifa Haftar dhidi ya serikali iliyotambuliwa rasmi na jamii ya kimataifa.

Shirika la EuroMed Rights limashiria kuwa serikali ya Imarati inawatumia mamluki wa Kisudani katika vita dhidi ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Libya na imeituhumu Abu Dhabi kuwa imefanya ukiukaji wa kutisha wa haki za binadamu.

Ripoti ya EuroMed Rights inasema kuwa, mamluki wa Kisudani walioajiriwa na Imarati wanasimamia jela na magereza, kuua raia kufanya magendo ya binadamu.

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limesema serikali ya Imarati inahusika moja kwa moja katika ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na mamluki wa Kisudani nchini Libya.

Nchi za Misri, Saudi Arabia na Imarati zinaendelea kumsaidia mbabe wa kivita Khalifa Haftar kusonga mbele katika jitihada zake za kuuteka mji mkuu wa libya, Tripoli. Mashambulizi hayo ya Haftari yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 1090 na kujeruhi melfu ya wengine.

Askari mamluki wa Sudan aliyeuawa Yemen

Katika wiki za hivi karibuni Wasudan wamekuwa wakiandamana kupinga hatua ya Saudi Arabia na Imarati ya kuwaajiri vijana wa nchi hiyo na kuwatuma kama wapiganaji mamluki katika nchi za Libya na Yemen.

Mamia ya askari na mamluki wa Kisudan wameuawa katika vita hivyo hususan huko Yemen.

Tags

Maoni