Feb 16, 2020 08:12 UTC
  • Kuidhinishwa na Bunge Baraza jipya la Mawaziri nchini Algeria

Katika hali ambayo, malalamiko na maandamano ya wananchi wa Algeria yanaendelea kushuhudiwa, Wabunge wa nchi hiyo wamepasisha kwa wingi wa kura majina ya Baraza la Mawaziri yaliyopendekezwa na Waziri Mkuu Abdul-Aziz Djerad na kwa msingi huo kulipatia kura ya kuwa na imani nalo baraza lake hilo.

Hili ni baraza la kwanza la mawaziri, tangu kuondolewa madarakani aliyekuwa rais wa muda mrefu wa Algeria Abdul-Aziz Bouteflika. Baraza hilo jipya la mawaziri linatarajiwa kuanza rasmi shughuli zake wiki ijayo. Baraza jipya la Mawaziri la Ageria lina mawaziri watano wanawake, huku Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni, Mambo ya Ndani na Sheria wakibakishwa katika nafasi zao.

Abdul-Aziz Djerad, Waziri Mkuu mpya wa Algeria ambaye aliteuliwa na Rais Abdul-Majid Tebboune na kukabidhiwa jukumu la kuunda serikali, aliwasilisha orodha ya mawaziri wake Bungeni akieleza nia ya kuyatafutia ufumbuzi matatizo ya kiuchumi na kijamii ya nchi hiyo na kuwataka wananchi wa Algeria kumsadia kwa ajili ya kufikia lengo hilo.

Djerad amesema: Tunapaswa kutumia nguvu zetu zote za kitaifa, shakhsia wa nchi na wananchi wake kwa waume na kushirikiana ili tuweze kukivuka kipindi hiki kigumu na hivyo kuzishinda changamoto za kiuchumi na kijamii.

Serikali mpya ya Algeria inatarajiwa kuanza shughuli zake katika hali ambayo, malalamiko na maandamano ya wananchi wa nchi hiyo yangali yanaendelea kushuhudiwa katika miji mbalimbali ya nchi hiyo.

Abdelmadjid Tebboune Rais mpya wa Algeria

Kuanzia Februari 22 mwaka jana, Algeria imekuwa ikishuhuudia maandamano ya kila Ijumaa ambapo wananchi hujitokeza barabarani na kulalamikia  mabaki ya utawala wa zamani wa nchi hiyo aliyelazimika kujiuzulu Abdul-Aziz Bouteflika.

Waandamanaji nchini Algeria  wanataka mabadiliko ya kimsingi katika mfumo wa utawala nchini Algeria; matakwa ambayo hadi sasa yamepuuzwa na viongozi walioko madarakani, kwani watawala wa Algiers hawajayatekeleza. Kuachiliwa huru watu waliotiwa mbaroni, vita dhidi ya ufisadi na kuondolewa madarakani baadhi ya viongozi wa serikali ambao ni mabaki ya utawala wa Bouteflika ni baadhi ya matakwa ya waandamanaji nchini Algeria.

Katika maandamano yao ya hivi karibuni ya Ijumaa iliyopita ya Februari 14, kwa mara nyingine tena wananchi hao sambamba na kusisitiza ulazima wa kuachiliwa huru watu waliotiwa mbaroni hivi karibuni, walipiga nara wakisema: "Tunataka Serikali ya Kitaifa na Sio Serikali ya Kijeshi" na Hatutaacha Kuandamana".

Waandamanaji nchini Algeria wanaamini kuwa, uchaguzi wa Rais uliofanyika nchini humo Disemba 12 mwaka jana kwa ajili ya kumchagua mtu wa kurithi mikoba ya Abdul-Aziz Bouteflika ulikuwa na lengo la kuhuisha serikali ya zamani ili kupitia uchaguzi huo watu wa Bouteflika waimarishe nguvu zao kupitia mfumo na utawala mpya na kisha waendeleze siasa na sera zile zile za utawala uliotangulia.

Abdul-Aziz Bouteflika, Ras wa zamani wa Algeria

Ni kutokana na sababu hiyo, ndio maana katika maandamano yao ya kila wiki, wananchi wa Algeria wamekuwa wakitoa nara za kutaka mageuzi ya kimsingi katika mfumo wa utawala nchini humo na kuachiliwa huru wafungwa wa kisiasa na kiitikadi na kwamba, hayo ni masharti ya kufanya mazungumzo na serikali.

Baada ya Rais Abdul-Majid Tebboune kula kiapo alitoa wito wa mazungumzo na wapinzani ili kurahisisha njia ya ustawi wa pande zote kiuchumi na kisiasa. Hata hivyo hadi sasa takwa hilo limekataliwa na wapinzani.

Nuruddin Bukeis, mhadhiri wa elimu-jamii (sosiolojia) katika Chuo Kikuu cha Algiers anaamini kuwa, Rais Abdul-Majid Tebboune hana budi isipokuwa kuwaita katika meza ya mazungumzo wapinzani wa kisiasa nchini humo ambao kimsingi ni wapinzani wa Bouteflika, hata hivyo madhali hajaweza kuwawekea wazi na bayana wananchi wa nchi hiyo sera na siasa zake, hapana shaka kuwa,  wito wake huo utaendelea kukabiliwa na upinzani.

Maandamano ya wananchi wa Algeria ambayo hufanyika kila Ijumaa lengo likiwa ni kutaka mageuzi katika mfuumo wa utawala nchini humo

Filihali, baada ya kipindi kirefu cha mgogoro wa kisiasa na kijamii, baraza jipya la mawaziri nchini Algeria linatarajiwa kushika hatamu za uongozi. Hata hivyo kuweko nyuso kama Sabri Boukadoum, Waziri wa Mashauri ya Kigeni, Belkacem Zaghmati, Waziri wa Sheria na Salah Eddine Dahmoune, Waziri wa Mambo ya Ndani na Serikali za Mitaa ambazo zimebakizwa katika nafasi zao kwenye baraza jipya la mawaziri, ni jambo ambalo wapinzani hawataweza kulivumilia.

Licha ya kuwa, viongozi wa Algeria wana matumaini kwamba, kuanza kazi baraza jipya la mawaziri kutapelekea kupungua malalamiko na kurejea utulivu nchini humo, lakini inaonekkana hilo ni jambo lililo mbali kwani wapinzani nchini humo hawako tayari kufumbia macho matakwa yao ya kisiasa na ya kimsingi ambayo wamekuwa wakiyalilia kwa miaka mingi sasa.

Tags

Maoni