Feb 18, 2020 16:42 UTC
  • Dk Vicent Mashinji
    Dk Vicent Mashinji

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama kikuu cha upinzani cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania Dk Vicent Mashinji leo Jumanne Februari 18 amehamia chama tawala CCM na kupokewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole.

Dk Mashinji amejiunga na chama tawala CCM katika ofisi ndogo za chama hicho zilizopo mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam ikiwa imepita miezi miwili tangu ufanyike mkutano mkuu wa Chadema na Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe kutompendekeza tena kuwa Katibu Mkuu.

Dk Mashinji katika sare za CCM pamoja na Humphrey Polepole Katibu  wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho tawala

Badala yake, Mbowe alimpendekeza mbunge wa Kibamba, John Mnyika kuwa Katibu Mkuu wa tano wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania kupigiwa kura na Baraza Kuu. Baada ya kukosa nafasi hiyo, Dk Mashinji alieleza masikitiko yake kwamba alitamani kuendelea kuwa Katibu Mkuu ili aweze kumalizia mipango aliyokuwa nayo ikiwemo maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020. Akiwa katika ofisi ndogo za CCM mtaa wa Lumumba, Dk Mashinji alisema: "Nimuombe Mwenyekiti wa CCM Rais John Magufuli kama ataridhia anipe nafasi ya kujiunga na CCM ili niweze kuchangia maendeleo ya nchi yangu." Ameongeza kuwa  CCM ina nia ya kuwapa wananchi maendeleo tofauti na chama alichotoka. "Ninaona kabisa CCM kiko tayari kuwaendeleza Watanzania na kule nilikotoka huo utayari siuoni." Hatua hii ya DK. Mashinji imekuja siku kadhaa tuu baada ya kinara mwingine wa Chadema, Frederick Sumaye kukihama chama hicho na kurejea CCM.

Sumaye katika ofisi za CCM, Dar es Salaam

Desemba 4, 2019, Sumaye alitangaza kuachana na chama cha upinzani cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akidai kuwa hakuna demokrasia ndani ya chama hicho baada ya kushindwa katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani. 

Mpama mwaka jana Waziri Mkuu wa zamani nchini Tanzania ambaye alikuwa mgombea urais kupitia tiketi ya chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edward Ngoyai Lowassa pia alikiasi chama hicho na kutangaza uamuzi wa kurejea chama tawala, CCM.

 

Tags

Maoni