Feb 19, 2020 05:55 UTC
  • Mkwamo katika kuunda serikali nchini Tunisia

Siku moja baada ya Harakati ya al-Nahdha kutangaza kutoshiriki katika serikali ya Waziri Mkuu mpya Elyes Fakhfakh, Rais Kais Saied ametangaza habari ya uwezekano wa kufanyika uchaguzi wa kabla ya wakati endapo Waziri Mkuu huyo mpya atashindwa kuunda baraza la mawaziri.

Harakati ya Nahdha imetangaza kuwa, wawakilishi wake katika Bunge la Tunisia hawatalipigia kura ya kuwa na imani nalo Baraza la Mawaziri la Fakhfakh. Pamoja na hayo, juhudi na mashauriano ya kuunda serikali mpya nchini Tunisia yangali yanaendelea.

Matukuio haya yanatokea miezi kadhaa baada ya kufanyika uchaguzi wa rais na Bunge nchini Tunisia ambapo Kais Saied aliibuka mshindi na kuwa Rais mpya wa nchi hiyo. Katika kinyang'anyiro cha Bunge, Chama cha al-Nahdha kilizoa viti vingi vya Bunge na hivyo kuifanya anga ya siasa nchini Tunisia kuwa tata.

Baada ya Habib al-Jemli aliyekuwa Waziri Mkuu mteule kushindwa kupata kura za kuwa na imani naye katika Bunge la nchi hiyo, Elyes Fakhfakh aliteuliwa na kupewa jukumu la kuunda serikali. Sera na utendaji wa Fakhfakh ni kujitenga mbali na aina yoyote ya mizozo na mivutano ya kisiasa na kujikita zaidi katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili serikali katika uwanja wa kiuchumi na kijamii. Pamoja na hayo, hatua zilizochukuliwa na Elyes Fakhfakh hazikukiridhisha Chama cha al-Nahdha ambacho ndicho chenye viti vingi katika Bunge la Tunisia.

Rais Kais Saied

Abdul-Karim al-Haruni, mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi wa al-Nahdha amesema kuwa, hakuna chama au kundi lolote la kisiasa linalopaswa kuwekwa kando na serikali, bali serikali mpya inapaswa kujumuisha vyama na mirengo yote ya kisiasa iliyoko Bungeni. Chama cha al-Nahdha hakitaipigia kura ya kuwa na imani nayo serikali mpya ya Tunisia kwa sababu, wizara zilizoanishwa na Waziri Mkuu Fakhfakh kwa ajili ya Nahdha katika serikali yake, hazitoi majibu ya uwiano wa kisiasa katika Bunge la nchi hiyo.

Kutokuweko mashauriano katika mchakato wa kuchagua mawaziri, kutokishirikisha Chama cha Qalb Tounes katika kuunda serikali kikiwa chama cha pili kwa ukubwa katika Bunge la Tunisia na kuongezeka mivutano baina ya Chama cha al-Nahdha na baadhi siasa za Rais Kais Saied zinatajwa kuwa sababu za kujitoa al-Nahdha katika serikali ijayo; uamuzi ambao unaweza kuitumbukiza Tunisia katika mgogoro mkubwa.

Baada ya Chama cha al-Nahdha kutangaza kuujitoa katika serikali ijayo, Waziri Mkuu Elyes Fakhfakh amehutubia kwa njia ya televisheni na kusema kuwa, Nahdha imechukua uamuzi wa kujitoa kutokana na kutoshirikishwa Chama cha Qalb Tounes katika serikali ya muungano, ili isiipigie kura ya kuwa na imani nayo serikali niliyopendekeza. Uamuzi huu ni hatari sana, kwani unaifanya nchi ikabiliwe na mazingira magumu.

Elyes Fakhfakh, Waziri Mkuu wa Tunisia

Kufuatia kujiondoa Chama cha al-Nahdhda katika serikali, sasa kumeanza kufanyika vikao mbalimbali vya mashauriano ya kisiasa nchini Tunisia. Moja ya mashauriano hayo ni mazungumzo yaliyofanyika kati ya Rached Ghannouchi Kiongozi wa Chama cha al-Nahdha na viongozi wa jumuiya za wafanyakazi na wafanyabiashara lengo likiwa ni kujaribu kuhitimisha mkwamo wa uundwaji wa serikali na kutafuta njia ya kufikiwa mwafaka. Mkwamo wa kisiasa nchini Tunisia umekuwa na taathira kwa hali ya uchumi wa nchi hiyo na hapana shaka kuwa, kwa hali hiyo matatizo ya kiuchumi yataongezeka zaidi.

Walid Luqini, mtafiti wa masuala ya kisiasa anasema: Ikiwa viongozi wa vyama na wa serikali hawatachukua maamuzi ya maana yenye lengo la kuikwamua Tunisia na mgogoro wa sasa, uchumi wa nchi hiyo utazidi kuzorota. Hivyo basi vyama vya siasa vinapaswa kutanguliza mbele maslahi ya kitaifa mbele ya maslahi ya kivyama na maslahi binafsi na kuzuia hatua yoyote ile inayolenga kushadidisha mivutano ya kisiasa.

Rais wa Tunisia ametahadharisha pia kuhusiana na kuvunjwa Bunge na kuitishwa uchaguzi wa kabla ya wakati. Filihali kuna mambo kadhaa ambayo yanaweza kufanyika ili kuikwamua Tunisia kutoka katika kinamasi ilichokwama.

Rached Ghannouchi Kiongozi wa Chama cha al-Nahdha

Mosi, ni Waziri Mkuu Elyes Fakhfakh kuendeleza mazungumzo na Chama cha al-Nahdha na hivyo kuandaa uwanja wa kukifanya chama hicho kiwe pamoja naye katika serikali ijayo. Pili, kama ilivyokuwa kwa Habib al-Jemli, naye Fakhfakh ajiuzulu ili Rais aitishe uchaguzi wa kabla ya wakati au amteue mtu mwingine na kumpa jukumu la kuunda Baraza la Mawaziri. Jambo jingine ni kufanya mazungumzo na vyama vingine na kufanya juhudi za kuunda serikali bila ya kukishirikisha Chama cha al-Nahdhda hatua ambayo itakuwa ni kukifuta chama hicho katika serikali, ingawa hilo nalo ni jambo gumu na lililo mbali mno.

Kupitia njia hizo ndipo mustakabali wa uongozi nchini Tunisia utakapofahamika ingawa njia bora kabisa ya kuupatia ufumbuzi mkwamo wa sasa wa kisiasa nchini Tunisia ni kupewa kipaumbele suala la kuweko ushirikiano mzuri wa vyama vyote na asasi mbalimbali na kutanguliza mbele maslahi ya kitaifa ili kwa hatuua hiyo njia ya kidemokrasia ambayo kwa kiwango fulani ilianza kuonekana baada ya mapinduzi ya umma ya 2011 kwa kuondolewa madarakani dikteta Zine El Abidine Ben Ali iweze kuendelea na kuwa kigezo cha kuigwa na nchi kama Misri na Libya.

Tags

Maoni