Feb 19, 2020 08:06 UTC
  • Baraza Kuu la Waislamu Kenya lamjia juu balozi wa Saudia nchini humo

Baraza Kuu la Waislamu nchini Kenya (SUPKEM) limekosoa vikali hatua ya balozi wa Saudi Arabia nchini humo, Mohammad Khayat ya kuingilia masuala ya uongozi wa baraza hilo.

Wanachama wa baraza hilo tawi la Pwani wakiongozwa na Mwenyekiti wa Muungano wa Vijana Waislamu, wamesema wameshangazwa na hatua ya mwanadiplomasia huyo wa Saudia kuingilia masuala ya ndani ya baraza hilo, kwa kupinga uongozi wa mwenyekiti wa sasa Hassan ole Naado.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Msikiti wa Mbaruku mjini Mombasa, Khamis Juma Mwaguzo, akiwa pamoja na wanachama wa baraza hilo kutoka Kwale, Likoni, Mvita, Changamwe na Kisauni, amesema, “jukumu letu ni kuhakikisha kwamba hatuendi kinyume na katiba ya SUPKEM."

Kiongozi huyo wa SUPKEM Pwani ya Kenya amefafanua kwa kusema, "tunajua balozi huyo anaelekezwa visivyo na watu fulani wala hatutaruhusu mwenyekiti wetu Hassan Ole Naado aondolewe ilhali alichaguliwa kwa mujibu wa katiba ya baraza hili.” 

 

 

Viongozi wa kisiasa na kidini Pwani ya Kenya

Ole Naado ambaye alikataa kuzungumzia suala hilo mbele ya waandishi wa habari tayari ameandika barua ya malalamiko kwa ubalozi wa Saudia Arabia nchini Kenya.

Sehemu ya barua hiyo ya Mwenyekiti wa SUPKEM kwa balozi wa Saudia inasema, “Mheshimiwa, masuala ambayo yamechochea kuandikwa kwa barua hii yanahusiana na mwenendo wako binafsi. Umekuwa ukitumia mbinu za kichinichini kushinikiza kuondolewa kwa mwenyekiti wa sasa ili nafasi yake ichukuliwe na mtu unayempendekeza, hatua ambayo sio ya kimaadili.” 

 

Tags

Maoni