Feb 19, 2020 10:45 UTC
  • Umoja wa Mataifa wataka kufanyike uchunguzi kuhusu mauaji ya hivi karibuni nchini Cameroon

Umoja wa Mataifa umeitaka serikali ya Cameroon ifanye uchunguzi kuhusiana na mauaji ya hivi karibuni katika jimbo linalozungumza Kiingereza katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika ambapo watu wasioungua 22 waliuawa kikatili wakiwemo watoto wadogo na wanawake wawili wajawazito.

Kupitia msemaji wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amewataka viongozi wa serikali ya Cameroon kuanzisha uchunguzi na kuchukua hatua muhimu ili waliohusika na jinai hiyo ya kutisha wafikiwe na mkono wa sheria.

Aidha Antonio Guterres ameeleza utayari wa Umoja wa Mataifa kufanya kazi na wadau wote nchini Cameroon ili kupata suluhisho la kisiasa la mzozo katika majimbo yanayozungumza Kiingereza nchini humo.

Watu wasiopungua 22 waliuawa Ijumaa iliyopita katika kijiji cha Ntumbo kwenye jimbo linalozungumza Kiingereza nchini Cameroon na makumi ya wengine kujeruhiwa.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu misaada ya kibinadamu (OCHA) katika majimbo ya Kaskazini-Magharibi na Kusini-Magharibi alinukuliwa akisema kuwa, miongoni mwa waliuawa yumo mwanamke mmoja aliyekuwa mjamzito na watoto 14 wakiwemo watano walio na umri wa chini ya miaka mitano.

Wazungumzaji wa Kiingereza wanaunda karibu asilimia 20 ya wakazi wote milioni 20 wa Cameroon, nchi ambayo lugha yake rasmi ni Kifaransa. Wazungumzaji hao wa Kiingereza wanalalamika kuwa wananyanyaswa na kutengwa na serikali kuu na wananyimwa haki zao kama raia wa Cameroon hivyo wanaona ni vyema wapiganie kujitenga.

Bunge la Cameroon tayari limeafiki kuwa maeneo yanayozungumza Kiingereza nchini humo yapewe hadhi maalumu katika hatua inayolenga kutuliza uasi wa wanaotaka kujitenga.

Tags

Maoni