Feb 20, 2020 13:09 UTC
  • Magaidi wa Al Shabab washambulia vituo viwili vya kijeshi Somalia

Magaidi wa kundi la Al Shabab wametekeleza mashambulizi dhidi ya vituo viwli vya Jeshi la Somalia katika eneo la Lower Shabelle na kuua askari wasiopungua wanne.

Kwa mujibu wa taarifa, shambulizi la kwanza lilijiri Jumatano katika kituo cha kijeshi cha el-Salini yapata kiliomita 55 kusini magharibi mwa mji mkuu, Mogadishu.

Msemaji wa Jeshi la Somalia Ismail Mukhtar amenukuliwa akisema wanajeshi wamefanikiwa kuwaua magaidi tisa katika shambulio hilo. Naye Kanali Hassan Mohamed Abukar amethibitisha kuwa wanajeshi wasiopungua wanne wameuawa katika hujuma hiyo.

Shambulizi la pili pia lilijiri Jumatano katika mji wa Qoryoley katika kituo cha kijeshi ambacho kinatumiwa na askari wa Jeshi la Somalia na wale wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika (AMISOM). Mji huo wa Qoryoley uko umbali wa kilimota 120 kutoka Mogadishu na ni maarufu kwa shughuli za kilimo.

Gavana wa Lower Shabelle Ibrahim Adan amewaambia waandishi habari kuwa magaidi watatu wa Al-Shabab wameuawa katika kituo hicho na kwamba hakuna askari yeyote wa Jeshi la Somalia au AMISOM aliyeuawa.

Magaidi wa Al Shabab

Jeshi la Somalia limesema limetekeleza oparesheni kadhaa katika eneo hilo na kukomboa vijiji vinne ambavyo vilikuwa vimetekwa na al-Shabaab.

Magaidi wa al-Shabaab wamekiri kuhusika na hujuma hizo mbili na kudai kuwa wameua askari 20 na kupora zana za kivita.

Kundi la kigaidi la al-Shabab lilianzisha hujuma zake nchini Somalia mwaka 2007 na limekuwa likiendesha ugaidi katika mji mkuu Mogadishu na maeneo mengine ya Somalia na pia katika nchi jirani ya Kenya. Magaidi hao walitumuliwa Mogadishu Agosti 2011 katika operesheni iliyofanywa na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika AMISOM, lakini limekuwa likifanya mashamabulizi ya kuvizia mara kwa mara.

Tags

Maoni