Feb 21, 2020 06:48 UTC
  • Safari ya Pompeo katika nchi kadhaa za Afrika na hamaniko la Marekani la kukabiliana na washindani wake

Muelekeo wa madola ya Magharibi kuhusiana na bara la Afrika daima umekuwa wa kulikoloni, kulinyonya na kulipora utajiri wake bara hilo, pamoja na kuwakandamiza Waafrika wanaopigania nchi zo kuwa huru na kujitawala.

Hata hivyo kudhoofika nguvu za madola ya kikoloni, kutokea mabadiliko ya msingi ya mahusiano na mazingira ya bara la Afrika; na muhimu zaidi ya yote, kuongezeka uwepo na ushawishi wa madola washindani wa Magharibi hasa China na Russia katika bara hilo, kumeihamanisha na kuitia tafrani Marekani ambayo ni kinara wa madola ya Magharibi.

Kwa muktadha huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo, wiki hii alifanya safari ya kuzitembelea nchi tatu za Afrika, ambazo ni Senegal, Angola na Ethiopia. Katika awamu ya mwisho ya safari yake hiyo, siku ya Jumanne Pompeo aliwasili Addis Ababa, ambapo katika hotuba aliyotoa katika mji mkuu huo wa Ethiopia alisisitiza kuwa, serikali ya Washington na mashirika ya Kimarekani ziko tayari kuimarisha uhusiano wa kibiashara na nchi za Kiafrika ili kuhakikisha watu wa nchi hizo wanakuwa na mustakabali wa matumaini na wa uhakika.

Pompeo (wa nne kulia) akiwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed mjini Addis Ababa

Masisitizo ya mara kwa mara ya Pompeo kuhusu utayarifu wa Marekani wa kusaidia kuimarishwa uhusiano na nchi za Kiafrika yanatolewa wakati serikali ya Trump imewawekea raia wa nchi kadhaa za bara hilo vizuizi vya kuingia nchini Marekani. Kinyume na madai ya waziri wake wa mambo ya nje, Rais wa Marekani hajaonyesha kuwa na hamu yoyote ya kuimarisha uhusiano wa nchi yake na bara la Afrika. Ijapokuwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson alifanya safari ya kulitembelea bara la Afrika mwanzoni mwa mwaka 2018, lakini baada ya kurejea Washington aliuzuliwa wadhifa wake huo na kuifanya safari yake hiyo isiwe na matunda yoyote kwa nchi za Afrika.

Kwa ujumla ni kwamba, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, serikali ya Trump haijaonyesha kulijali na kulizingatia kwa namna yoyote ile bara la Afrika. Hata matamshi ya kifidhuli aliyotoa rais huyo wa Marekani kuhusu nchi za Kiafrika na hatua yake ya kuwawekea vizuizi vya kuwapatia viza raia wa baadhi ya nchi za bara hilo vimeibua hisia hasi kuhusiana na siasa za Washington katika nchi hizo.  

Pompeo (kushoto) alipokutana na Rais Macky Sall wa Senegal mjini Dakar

Kabla Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani hajaanza safari yake ya kuzitembelea nchi za Afrika, Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo Mark Esper alitangaza kuwa, kwa kutenga suhula mpya, Washington itavipanga upya vikosi vya majeshi yake barani Afrika kwa ajili ya kukabiliana na ushawishi  wa China na Russia na kwamba idadi ya askari wa Marekani walioko barani humo itapunguzwa kwa kiwango kikubwa. Afrika ni miongoni mwa maeneo ambayo Marekani imepanga kuangalia upya uwepo wa askari wake kuliko maeneo mengine.

Lakini pamoja na hayo, inaonesha moja ya sababu muhimu za safari ya Pompeo katika nchi za Afrika ni kujaribu kukabiliana na ushawishi wa madola mapya yenye nguvu za kiuchumi na washindani wa kibiashara na kijeshi wa Washington, yaani China na Russia. Katika siku za karibuni, waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani ameonyesha msimamo mara kadhaa dhidi ya uwepo wa mashirika ya Kichina, hususan barani Afrika. Hata hivyo, katika nchi alizotembelea Pompeo  ikiwemo Ethiopia, Wachina wameshawekeza na kutekeleza mamia ya miradi mbali mbali ya kiuchumi.

Licha ya nchi za Afrika kupata uhuru, Wamagharibi, wakiongozwa na Marekani, wangali wanafanya juu chini kuhakikisha wanajiimarisha na kuendelea kuwepo kisiasa na kiuchumi barani humo, kupitia ushawishi wanaojijengea katika miundo ya kisiasa, kiuchumi na hata ya kijeshi ya nchi za Kiafrika. Rais Vladimir Putin wa Russia anaizungumzia hali hiyo kwa kusema: Tunashuhudia baadhi ya nchi za Magharibi zinavyoamiliana na serikali za nchi za Kiafrika kwa mashinikizo na kuzirubuni kwa vitisho. Kwa kutumia njia hizo zinajaribu kurejesha satua na ushawishi wao kwa makoloni yao ya zamani, tab'an kwa kutumia mbinu mpya.

Rais Vladimir Putin wa Russia (anayepunga mkono) katika picha ya pamoja na viongozi wa Afrika baada ya mkutano wa kiuchumi wa Russia na Afrika

Pamoja na yote hayo, katika miaka ya hivi karibuni na sambamba na kutokea mabadiliko makubwa katika miundo ya kiuchumi duniani na kujitokeza madola mapya yenye nguvu za kiuchumi, mgao wa nchi za Magharibi ikiwemo Marekani katika soko la biashara la nchi za Kiafrika umepungua. Na katika mazingira hayo, madola mapya yenye nguvu za kiuchumi kama China, India, Brazil na pia Russia yamegeuka kuwa washirika wakuu wa kibiashara wa nchi za bara la Afrika.

Kutokana na kuongezeka uwezo wa bara la Afrika kwa upande wa rasilimaliwatu na maliasili pamoja na Afrika kuwa na utajiri mkubwa wa nishati na madini, hivi sasa bara hilo linajizatiti na kuimarisha taratibu nafasi yake katika mlingano wa nguvu kimataifa na hivyo kuzidi kuyavutia madola makubwa katika uga wa kimataifa. Hali hiyo imeibua mchuano mkali kati ya madola hayo, wa kupigania kuwa na uwepo na ushawishi mkubwa zaidi ndani ya bara hilo.

Ukweli ni kwamba, licha ya Washington kufanya juu chini ili kupunguza ushawishi wa China na Russia, tukiuangalia mwenendo wa mahusiano ya Beijing na Moscow na nchi za Kiafrika tutabaini kuwa mahusiano hayo katika nyuga mbali mbali yanazidi kustawi na kuimarika.../  

Tags

Maoni