Feb 21, 2020 14:54 UTC
  • UN: Mazungumzo ya usitishaji vita Libya yameanza tena mjini Geneva

Umoja wa Mataifa umetangaza leo kuwa, mazungumzo ya usitishaji vita nchini Libya baina ya vikosi vinavyopigania kuudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli, yameanza tena mjini Geneva, Uswisi siku kadhaa baada ya serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa kujitoa kwenye mazungumzo hayo kufuatia hatua ya mrengo hasimu ya kushambulia bandari ya Tripoli.

Taarifa hiyo ya Umoja wa Mataifa imetolewa bila kupatikana maelezo yoyote kutoka Serikali ya Muafaka wa Kitaifa (GNA) ambayo ilijiondoa kwenye mazungumzo hayo siku ya Jumanne.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Rheal LeBlanc, amewaeleza waandishi wa habari mjini Geneva kwamba, mazungumzo hayo yalianza tena jana na yataendelea leo. 

Hayo yanajiri huku mrengo hasimu wa GNA wa kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya (LNA) linaloongozwa na Khalifa Haftar ukisisitiza kuwa, usitishaji vita utawezekana pale tu Uturuki na wapiganaji kutoka Syria watakapositisha uungaji mkono wao kwa Serikali ya Muafaka wa Kitaifa.

Uturuki imechukua hatua ya kuisaidia na kuiunga mkono GNA ili kukabiliana na hujuma za mrengo wa Haftar wa LNA unaoungwa mkono na Imarati na Misri.

Khalifa Haftar

Katika mahojiano aliyofanya leo na shirika la habari la Russia la RIA, Haftar amesema, usitishaji mapigano utafikiwa baada ya kutimizwa masharti kadhaa, ikiwa ni pamoja na kile alichosema kuondoka mamluki wa Kisyria na Kituruki, kukomesha Uturuki utoaji silaha inazoipatia serikali ya muafaka wa kitaifa na kutokomezwa makundi ya kigaidi katika mji wa Tripoli.

Itakumbukwa kuwa mnamo mwezi Aprili, 2019, vikosi vya Khalifa Haftar  vilianzisha hujuma na mashambulio dhidi ya Tripoli kwa lengo la kuuteka mji mkuu huo wa Libya unaodhibitiwa na Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya nchi hiyo inayotambuliwa rasmi kimataifa.../ 

 

 

Tags

Maoni