Feb 22, 2020 02:47 UTC
  • Thomas Thabane
    Thomas Thabane

Waziri Mkuu wa Lesotho, Thomas Thabane alikosa kufika mahakamani jana Ijumaa kwa ajili ya kesi ya mauaji inayomuandama, kutokana na kile kilichotajwa na familia yake kama sababu za kiafya. Polisi ya nchi hiyo siku ya Alkhamisi ilisema kiongozi huyo angeshtakiwa rasmi jana Ijumaa kwa mauaji ya mke wake wa zamani.

 Potlako Thabane, mtoto wa kiume wa Thabane amesema Waziri Mkuu huyo amepelekwa nchini Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu, na wala hajakimbia nchi na mashitaka yanayomkabili kama inavyoripotiwa kwenye mitandao ya kijamii.

Naibu Kamishna wa Polisi, Paseka Mokete amesema iwapo Waziri Mkuu huyo atajaribu kukimbia mkono wa sheria, basi vyombo vya usalama vitatoa waranti ya kumkamata. Waziri Mkuu huyo wa Lesotho tayari ametangaza kuwa atajiuzulu wadhifa wake huo. 

Mke wa zamani wa Waziri Mkuu huyo wa Lesotho, Lipolelo Thabane, 58, aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya gari lake mnamo Juni 14 mwaka 2017 alipokuwa anarudi nyumbani huko Maseru, mji mkuu wa Lesotho.

Siku mbili baadaye, mumewe, Thomas Thabane aliteuliwa rasmi kuwa Waziri Mkuu wa Lesotho. Kabla ya Lipolelo kuuawa hapo mwaka 2017, mke huyo wa zamani wa Waziri Mkuu wa Lesotho na mumuwe walikuwa katika mchakato wa kutalikiana.

Waziri Mkuu wa Lesotho na mkewe wanaandamwa na mashitaka ya mauaji

Mapema mwezi huu, Maesaiah Thabane, mke wa sasa Waziri Mkuu huyo wa Lesotho alipandishwa kizimbana akihusishwa pia na mauaji hayo lakini aliachiwa huru kwa dhamana.

Maesaiah na Waziri Mkuu wa sasa wa Lesotho, Thabane Lipolelo walioana miezi miwili baada ya tukio hilo la kupigwa risasi na kuuawa Lipolelo Thabane. 

Tags

Maoni