Feb 23, 2020 13:36 UTC
  • UN na IGAD zapongeza uundwaji wa serikali mpya Sudan Kusini

Jumuiya ya Maendeleo ya Serikali ya Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) na Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Afrika (UNHCR) zimepongeza hatua ya kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na shauku huko Sudan Kusini.

Filippo Grandi, Kamishna wa UNHCR amesema katika taarifa kuwa, serikali mpya inahuisha matumaini ya amani na mustakabali mzuri kwa watu wa nchi hiyo ambao wameteseka kutokana na mgogoro wa muda mrefu.

Nayo IGAD imeahidi kuendelea kuiunga mkono serikali ya Juba ili kuhakikisha kuwa taifa hili linakuwa na amani ya kudumu, utulivu na ustawi. Umoja wa Afrika pia umepongeza hatua ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kiataifa nchini Sudan Kusini.

Hatimaye baada ya ngoja ngoja, Serikali ya Umoja wa Kitaifa huko Sudan Kusini iliundwa hapo jana baada ya kinara wa upinzani, Riek Machar kuapishwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Salva Kiir.

Filippo Grandi, Kamishna wa UNHCR 

Kwa mujibu wa mkataba wa amani uliofikiwa kati ya pande mbili, Rais atakuwa ni mmoja, lakini atakuwa na makamu watano huku mawaziri wakiwa 35. Aidha kutakuwa na wabunge 550 huku Magavana wakiwa 10 katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.

Uamuzi wa Rais Kiir kukubali kupunguzwa kwa idadi ya majimbo kutoka 32 hadi 10 na Machar kuhakikishiwa usalama, ni miongoni mwa sababu kubwa ambazo zimefanikisha uundwaji wa serikali hiyo.

Tags

Maoni