Feb 26, 2020 13:44 UTC
  • Makumi wauawa katika ghasia za kabla ya uchaguzi Burundi

Serikali ya Burundi imekiri kuua watu 22 ndani ya siku chache zilizopita, kwa tuhuma za kufanya 'makosa' yanayohusishwa na uchaguzi mkuu ujao.

Vyombo vya dola nchini humo vimeripoti kuwa, watu hao waliuawa katika mji mkuu Bujumbura, na kwamba maafisa wawili wa polisi wameuawa pia katika ghasia hizo za kabla ya uchaguzi.

Vyombo vya usalama nchini Burundi vimesema kuwa, vimewatia mbaroni watu sita wanaohusishwa na uhalifu huo wa kabla ya uchaguzi unaotazamiwa kufanyika mwezi Mei mwaka huu.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini humo, Pierre Nkurikiye amethibitisha habari ya kutokea mauaji hayo katika wilaya za Nyabiraba na Isare viungani mwa Bujumbura na kuonya kuwa, "tutakabiliana na watenda jinai wanaotaka kutumia vibaya mazingira haya ya uchaguzi. Wananchi wawe watulivu kwani maafisa usalama wamedhibiti mambo."

Maafisa wa polisi Burundi wakimshambulia raia

Wananchi wa Burundi wanatazamiwa kushiriki uchaguzi mkuu hapo mwezi Mei mwaka huu kumchagua mrithi wa Rais Pierre Nkurunziza ambaye yuko madarakani tokea mwaka 2005. 

Chama tawala CNDD-FDD tayari kimemteua Katibu Mkuu wa chama hicho Jenerali Evariste Ndayishimiye kuwa mgombea wake katika uchaguzi wa rais, huku chama kikuu cha upinzani nchini humo cha National Congress for Liberty (CNL) kikimuidhinisha Agathon Rwasa kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi huo wa Mei 20.

 

Tags

Maoni