Mar 06, 2020 11:34 UTC
  • Vifaa vya tiba vya kujikinga na Corona vya magendo vyanaswa Morocco vikipelekwa Ulaya

Vyombo vya habari vya Morocco vimeripoti kwamba, maafisa wa nchi hiyo wamenasa maelfu ya maski za masuala ya tiba zilizokuwa zikitoroshwa na kupelekwa Ulaya.

Gazeti la al Quds al Arabi linalochapishwa London limeripoti kuwa, raia mmoja wa Uingereza amekamatwa katika uwanja wa ndege wa Agadir huko kusini magharibi mwa Morocco akijaribu kutorosha maski elfu 16 na kuzipelekea Manchester kwa njia za magendo. 

Vilevile maafisa wa forodha wa Morocco wamenasa shehena nyingine iliyokuwa na vifaa vya tiba vya maski laki moja katika bandari ya Tangier. Vifaa hivyo vilikuwa vikisafiishwa kwa njia za magendo kuelekea katika nchi za Ulaya. 

Vifaa vya tiba vinatoroshwa kutoka Morocco kwenda Ulaya

Kasi ya maambukizi ya virusi vya Corona katika nchi za Ulaya imesababisha uhaba mkubwa wa baadhi ya vifaa vya tiba husuan maski na dawa za kuosha mikono kwa ajili ya kujikinga na virusi hivyo na suala hili linatajwa kuwa sababu ya kushamiri biashara ya magendo ya vifaa hivyo. 

Morocco ni miongoni mwa nchi za Kiafrika zilizoripoti kesi za maambukizi ya kirusi cha Corona. Shughuli na mikusanyiko yote ya michezo na masuala ya kiutamaduni zimepigwa marufuku nchini humo kwa kuhofia maambukizi zaidi ya virusi vya Corona. 

Tags

Maoni