Mar 24, 2020 13:30 UTC
  • Kukaribisha Umoja wa Mataifa makubaliano ya usitishaji vita katika vita vya ndani nchini Libya

Vita vya ndani nchini Livya viliibua wasiwasi mkubwa kufuatia mashambulio ya mara kwa mara ya Jeshi la Taifa la Libya linaloongozwa na jenerali Khalifa Haftar yaliyoanza Aprili mwaka jana kwa shabaha ya kuiangusha Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa.

Aidha vita hivyo vilichukua mkondo mpya kufuatia uungaji mkono wa madola ya kigeni kwa pande mbili zinazozozana katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Pamoja hayo, kusambaa kwa virusi vya Corona kulipelekea kujitokeza matukio muhimu katika uwanja huo. Udharura wa kukabiliana na maradhi ya Covid-19 yanayosababishwa na virusi vya Corona yanayotishia pande zote hasimu nchini Libya ni jambo lililomfanya jenerali muasi Khalifa Haftar na Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ziridhie kusitisha vita.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekaribisha kwa mikono miwili jibu chanya la serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya na la wanamgambo wanaoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar kwa ajili ya kusimamisha mapigano nchini humo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, anataraji kuwa majibu hayo yatapelekea kusitishwa mapigano katika nchi hiyo haraka iwezekanavyo na bila ya masharti yoyote.

Mapigano nchini Libya

Katika taarifa yake rasmi, Antonio Guterres amezitaka pande hasimu nchini Libya zizingatie mazingira magumu ya kibinadamu nchini humo na taathira tarajiwa ya virusi vya Corona na hivyo zichukue hatua za lazima za kukabiliana na virusi hivyo na kudhamini suala la upelekaji misaada ya kibinadamu bila vizingiti katika maeneo tofauti ya nchi hiyo.

Stephane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alitangaza katika taarifa yake Jumamosi iliyopita kwamba: Antonio Guterres anazitaka pande hasimu nchini Libya ziweke chini silaha zao na zikubaliane na rasimu ya muda ya makubaliano ya usitishaji vita iliyozungumziwa na Kamisheni ya Kijeshi ya Pamoja ya Libya ya 5+5 katika kipindi cha kuenea virusi vya Corona.

Hadi sasa kumefanyika juhudi mbalimbali za kimataifa kwa shabaha ya kuhitimisha vita vya ndani nchini Libya. Moja ya juhudi hizo ni mkutano wa Januari 13 mwaka huu wa wawakilishi wa Uturuki, Russia na pande hasimu nchini Libya uliofanyika mjini Moscow na kumalizika bila ya natija, ambapo Khalifa Haftar aliondoka katika mji huo bila kusaini hati ya makubaliano. Khalid al-Mishri, Mkuu wa Baraza Kuu la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya anasema kuwa, Imarati ndio iliyokwamisha kufikiwa usitishaji vita katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Katika hatua iliyofuata, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel aliitisha mkutano  wa Berlin kuhusu Libya Januari 19 mwaka huu ambapo Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi 11, marais, viongozi wa ngazi za juu wa Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu walishiriki katika mkutano huo. Katika taarifa ya mwisho ya mkutano huo, washiriki waliahidi kudhamini usalama wa taasisi za mafuta za Libya kama ambavyo waliahidi pia kutoingilia kati mapigano ya ndani ya nchi hiyo. Waidha waliahidi kwamba, wangezitaka pande zote za kimataifa kuchukua hatua kama hizo. Kadhalika ilisisitizwa kuzuia moja kwa moja hatua za kihasama na ulazima wa kupunguza mzozo na kupatikana usitishaji vita.

Pamoja na hayo vikosi vya wanamgambo wanaoongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar vinavyojiita Jeshi la Taifa la Libya vilianzisha tena mashambulio yao dhidi ya mji mkuu Tripoli na kimsingi vikawa vimepuuza makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa Berlin. Baada ya hapo kukafanyika mkutano wa siku moja tarehe 16 ya mwezi uliopita wa Februari huko Munich Ujerumani kwa minajili ya kufuatilia matokeo na makubaliano ya mkutano wa Berlin. Mada ya mkutano huo maalumu, ilikuwa ni kutekeleza usitishaji vita nchini Libya na ulazima wa kutekelezwa vikwazo vya silaha katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Ghassan Salame, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya

Licha ya kuweko juhudi mbalimbali, lakini mapigano nchini Libya yangali yanaendelea kutokana na himaya na uungaji mkono wa pande zote wa nchi mbalimbali kwa pande mbili zinazopigana katika nchi hiyo. Hivi sasa jenerali Khalifa Haftar ameongeza juhudi zake maradufu zenye lengo la kuikalia kwa mabavu Tripoli. Lengo la Haftar ni kuidhibiti Libya yote. Hata hivyo hadi sasa ameshindwa kufikia malengo yake hayo. Ghassan Salame, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya amesema: Hali ya mambo nchini Libya ni tata sana.

Ukweli wa mambo ni kuwa, kuendelea vita vya sasa nchini Libya baina ya Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa na vikosi vya Khalifa Haftar kumetokana na kuendelea himaya na uungaji mkono mkubwa wa madola ya kigeni kwa pande mbili hizo. Kwa msingi huo basi, hatua ya awali kabisa na ya kweli ya kupunguza mzozo wa sasa wa Libya na mapigano yanayoendeea katika nchi hiyo ni mataifa husika yanayoziunga mkono pande hizo kuacha kufanya hivyo, kuweko usitishaji vita na hatimaye kuanza mazungumzo ya kisiasa kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa sasa wa nchi hiyo.  Inaonekana kuwa, filihali virus vya Corona vimezifanya pande mbili nchini Libya ziridhie kusitisha vita na mapigano.

Tags

Maoni