Mar 25, 2020 13:21 UTC
  • DRC yatangaza hali ya dharura kwa ajili ya kukabiliana na virusi vya Corona

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza hali ya dharura na kuufunga mji mkuu wa Kinshasa au kujitenga katika hatua ya kupambana naa maambukizi ya virusi vya Corona.

Rais Félix Tshisekedi alitangaza kuchukua hatua hizo jana jioni kupitia televisheni ya taifa.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema kuwa, pamoja na kufunga mipaka ya nchi, kusitisha safari za ndani na nje ya mji mkuu zikiwemo za mabasi, ndege na majini, utekelezaji wa haraka unahitajika.

Mpaka sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeripotiwa kuwa na wagonjwa 48 wa covid-19 na watu watatu kufariki dunia kutokana na maambukizi ya ugonjwa huo.

Mji mkubwa wa pili wa taifa hilo, Lubumbashi, ulifungwa kwa saa 48-siku ya Jumatatu baada ya watu wawili kutambuliwa kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona.

Mmoja alikuwa mwanamume mwenye miaka 47 na mtoto wake wa kiume wa miaka 13, walikuwa wametokea mji mkuu wa Kinshasa siku ya Jumapili.

Na siku hiyo hiyo, kifo cha pili kilichotokana na ugonjwa wa corona kilitangazwa na Waziri wa Afya, Eteni Longondo huku wengine 30 walikutwa na maambukizi ya ugonjwa huo tangu March 10, 2020.

Gavana wa Lubumbashi alitangaza saa 48 kwa mji wa Lubumbashi kufungwa, kuanzia Jumatatu wakati wakijaribu kubaini abiria 75 ambao wanapaswa kutengwa.

Baadhi ya marufuku zilizowekwa na serikali ya Kinshasa ni teski kutobeba abiria zaidi ya watatu, mabasi ya umma ambayo yalikuwa yanabeba watu zaidi ya 60 na sasa yanaruhusiwa kubeba abiria 20 tu, kumbi zote za starehe pia zimefungwa, nyumba za ibada - makanisa yamefungwa, vyuo na shule zote zimefungwa na ndege za kimataifa zimepigwa marufuku isipokuwa ndege za mizigo na meli za mizigo.

 

 

Maoni