Mar 26, 2020 13:17 UTC
  • Magufuli: Mlipuko wa corona hautafanya uchaguzi mkuu wa Tanzania uakhirishwe

Rais John Magufuli wa Tanzania amesema uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu hautaakhirishwa licha ya kuwepo kwa mlipuko wa virusi vya corona.

Rais Magufuli amesema hayo leo Alkhamisi katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma wakati akipokea ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na ripoti ya Takukuru ambapo amesisitiza kuwa, uchaguzi utafanyika kama ilivyopangwa, kwa kuwa hakuna mtu anayependa kukaa ofisini muda mrefu.

Amesema, "na uchaguzi tutafanya, wapo wanaofikiri kwamba tutaahirisha, nani anataka kukaa kwenye maofisi haya muda wote huo?"

Mapema mwaka huu, Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisema kuwa, Serikali ya nchi hiyo imejipanga kuhakikisha kuwa, uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu unakuwa wa amani, huru na haki.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amesema mgonjwa wa kwanza nchini wa virusi vya corona, Isabela Mwampamba (46) ameshapona ugonjwa huo. Amesema, "tumeanza utaratibu wa kumruhusu kurudi nyumbani, jamii imkubali, impokee bila kumnyoshea vidole, bila kudhalilishwa, bila kutukanwa wala kudharauliwa" 

Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu

Ameongeza kuwa, mpaka sasa wasafiri 245 wametengwa kwenye vituo vilivyoandaliwa baada ya kuingia nchini humo wakitoka nchi zilizoathirika zaidi na virusi hivyo. Waziri wa Afya wa Tanzania amebainisha kuwa, hadi sasa Tanzania ina jumla ya wagonjwa 13 na tayari wasafiri zaidi ya milioni 1 wamekwishafanyiwa vipimo vya joto la mwili.

Hivi karibuni, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa alisema kuwa, serikali imeunda kamati tatu za kupambana na mlipuko wa corona, na kwamba inaendelea kufanya tathmini kuhakikisha inazuia virusi vya corona visiweze kusambaa kwa kiasi kikubwa nchini humo.  

Tags

Maoni