Mar 30, 2020 11:17 UTC
  • Al Shabab yatangaza kuhusika na shambulio lililoua mtu mmoja na kujeruhi wanne Somalia

Genge la kigaidi na ukufurishaji la al Shabab limetangaza kuhusika na shambulio lililopelekea mtu mmoja kuuawa na wengine wanne kujeruhiwa jana Jumapili. Gavana wa eneo moja ni miongoni mwa waliojeruhiwa katika shambulio hilo la kigaidi.

Kabla ya hapo Jeshi la Polisi la Somalia lilikuwa limetangaza kuwa watu watatu wamejeruhiwa baada ya mtu mmoja aliyekuwa amejifunga mabomu kujiripua katikati ya watu na maafisa wa kieneo katika jimbo la Puntland huko Somalia.

Hata hivyo taarifa za baadaye zimesema kuwa, kwa uchache mtu mmoja ameuawa na wengine wanne wamejeruhiwa akiwemo gavana wa eneo la Nugal, Abdisalan Hassan Hersi na mkuu wa zamani wa jeshi la polisi la mji huyo, Farah Galangoli wakati mtu aliyekuwa amejifunga mabomu alipojiripua katika mji wa Garowe. Habari hiyo imethibitishwa pia na afisa wa polisi wa eneo hilo, Mohamud Ahmed Guled.

Miripuko na mauaji ni janga kubwa Somalia ambalo haijulikani litaisha lini

 

Taarifa hiyo imesema kuwa, Abdisalan Hassan Hirsi na mkuu wa zamani wa polisi wa eneo la Nugal wamejeruhiwa vibaya katika shambulizi hilo na wamewahishwa hospitalini kwa ajili ya matibabu.

Afisa huyo wa polisi amesema, askari wa serikali walifika haraka kwenye eneo hilo la kuanza uchunguzi mara moja.

Mji wa Garowe ndiyo makao makuu ya jimbo la Puntland lililojitangazia utawala wa ndani na uko umbali wa kilomita 947 kaskazini mashariki mwa mji mkuu, Mogadishu. 

Tags

Maoni