Apr 02, 2020 02:23 UTC
  • Marekani yaendelea kuua raia katika mashambulizi yake ya anga Somalia

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema jeshi la Marekani linaendelea kuua raia wasio na hatia katika mashambulizi yake ya anga nchini Somalia.

Katika taarifa ya jana Jumatano, shirika hilo limesema raia wawili wa Somalia waliuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika hujuma za anga za Marekani mwezi Februari mwaka huu katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Abdullahi Hassan, baba ya raia aliyeuawa katika shambulizi la anga la Februari 2 katika mji wa Jilib yapata kilomita 112 kusini mwa Kismayo, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, "sijui sababu ya kuuawa binti yangu Nurto Kusow Omar Abukar aliyekuwa na umri wa miaka na kujeruhiwa dadake zake wawili wa miaka 7 na 12 pamoja na babu yao wa miaka 70. Na mimi pia wakitaka kuniua waniue, nipo sehemu ya wazi, siwaogopi!"

Aidha Februari 24, ndege isiyokuwa na rubani ya Marekani iliua raia mwingine kwa jina la Mohamud Salad Mohamud, mkulima wa ndizi katika kijiji cha Kumbareere, umbali wa kilomita 10 kutoka mji huo wa Jilib, huku mamake mzazi na mpwa wake wakijeruhiwa pia.

Mbali na hujuma za al-Shabaab, Somalia inaandamwa pia na mashambulizi ya anga ya US

Kama ilivyotarajiwa, Kikosi cha Jeshi la Marekani barani Afrika AFRICOM kimetoa taarifa na kudai kuwa, mashambulizi hayo ya 'drone' yalilenga maficho ya al-Shabaab na kwamba eti kinachunguza vifo vya raia hao wa Somalia.

Utafiti uliofanywa hivi karibuni na asasi isiyo ya kiserikali ya Hiraal yenye makao makuu yake mjini Mogadishu ulibainisha kuwa, mashambulizi ya anga yanayofanywa kila uchao na Marekani nchini Somalia yameshindwa kulitokomeza au hata kulidhoofisha kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab na badala yake yamekuwa na taathira hasi kwa raia wa kawaida.

 

 

 

 

Tags

Maoni