Apr 05, 2020 08:12 UTC
  • Wananchi wakosoa mpango wa kufanyia majaribio chanjo ya corona DRC

Wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamekosoa vikali mpango wa kufanyia majaribio chanjo ya corona nchini humo ambao serikali imeafiki.

Wakongomani wamekosoa mpango huo wakisisitiza kuwa, ni fedheha kwa serikali kuruhusu taifa hilo ligeuzwe 'panya wa maabara' katika kufanyia majaribio chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 (corona).

Siku ya Ijumaa, Jean-Jacques Muyembe, Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Biolojia anayeongoza jopokazi la kupambana na janga la corona nchini DRC alisema, "tumeteuliwa kufanya majaribio haya. Chanjo hiyo itazalishwa Marekani, Canada au China. Utafika wakati fulani ambapo itashindikana kudhibiti virusi vya corona, njia pekee ya kuidhibiti ni chanjo. Chanjo ndiyo iliyotusaidia kudhibiti Ebola."

DRC imeafiki mpango huo wakati huu ambapo shakhsia na taasisi za nchi za Afrika zimeendelea kukosoa matamshi ya madaktari wawili wa Ufaransa, ambao kwa kejeli na dharau, wamependekeza kufanyika majaribio ya chanjo ya corona barani Afrika. 

Maafisa wa afya wakitoa chanjo ya Ebola Butembo, Kongo DR

Pendekezo hilo la Wamagharibi la kuwageuza Waafrika 'panya wa maabara' linakuja katika hali ambayo, akthari ya kesi za zaidi ya milioni moja na laki mbili za ugonjwa wa Covid-19 (corona) zimeripotiwa Marekani na katika nchi za Ulaya.

Huku hayo yakiarifiwa, Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani  Afrika (CDC) kimesema kuwa, idadi ya watu walioaga dunia kutokana na virusi vya corona katika nchi 50 za bara hilo imefikia 313, huku idadi ya watu waliothibitishwa kuambukizwa virusi hivyo ifikia 7,741. Kadhalika watu 753 ambao walikuwa wameambukizwa virusi hivyo wamepona.

Tags

Maoni