Apr 06, 2020 08:06 UTC
  • AU yatahadharisha kuhusu tishio la corona kwa fursa za ajira barani Afrika

Umoja wa Afrika (AU) umetahadharisha kuwa janga la maambukizo ya virusi vya corona linahatarisha fursa milioni 20 za ajira barani humo.

Taarifa iliyotolewa na umoja huo, mbali na kutahadharisha kuhusu tishio la kirusi cha corona kwa fursa milioni 20 za ajira barani Afrika, imetabiri kuwa kutokana na mripuko wa kirusi hicho, kiwango cha biashara za nchi za bara hilo katika mwaka huu kitapungua kwa asilimia 35 kulinganisha na mwaka 2019 na kusababisha hasara ya dola bilioni 270.

Umoja wa Afrika umetangaza kuwa, idadi ya watu walioambukizwa COVID-19 barani humo hivi sasa imeshapindukia elfu nane.

Kiwango cha maambukizo ya virusi vya corona katika bara la Afrika kingali ni cha chini kulinganisha na maeneo mengine ya dunia, lakini maambukizi yake yanaendelea kuenea kwa kasi katika eneo hilo linalojulikana kama bara masikini zaidi duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom amewataka viongozi wa nchi za Afrika kuchukua hatua kamili na za pande zote kujiandaa na kile alichokiita kimbunga cha corona kinachokaribia kuvumia bara la Afrika.

Nchi nyingi za Afrika hazina miundombinu ya afya kwa ajili ya kukabiliana na corona, ambapo inakadiriwa kuwa kwa kila watu elfu kumi kuna daktari mmoja tu wa kuwahudumia.../

 

Tags

Maoni