Apr 06, 2020 13:12 UTC
  • Sudan yaipa Sudan Kusini msaada mwingine wa kijeshi kudhamini utekelezaji wa makubaliano ya amani

Serikali ya Sudan imetuma msaada wa tatu wa kijeshi kwa jirani yake wa kusini, Sudan Kusini ikiwa ni sehemu ya juhudi za kudhamini utekelezaji wa makubaliano ya amani baina ya serikali ya Juba na wapinzani.

Shirika rasmi la habari la Sudan (SUNA) limepoti habari hiyo na kuongeza kuwa, serikali ya Khartoum imeamua kutuma msaada wa tatu wa kijeshi kwa serikali ya Juba kulingana na makubaliano ya amani yaliyofikiwa baina ya serikali ya Sudan Kusini na wapinzani na kwa mujibu wa mapatano ya kuisaidia Sudan Kusini kulinda usalama wa wananchi wake. Msaada huo wa tatu na wa mwisho wa kijeshi ulitumwa jana Jumapili nchini Sudan Kusini kutokea Khartoum.

Adil Ibrahim, Balozi wa Sudan mjini Juba amesema kuwa, hiyo ndiyo shehena ya mwisho ya misaada ya kijeshi ya Sudan kwa Sudan Kusini kufuatia shehena mbili za misaada hiyo zilizotumwa huko nyuma kwa serikali ya Juba.

Mahasimu wawili Salva Kiir na Riek Machar wakinyanyuliwa mikono mjini Khartoum Sudan baada ya kufikiwa makubaliano ya amani ya Sudan Kusini

 

Itakumbukwa kuwa serikali ya Khartoum inalazimika kuisaidia Sudan Kusini kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata dhamana ya kutekelezwa makubaliano ya amani baina ya serikali ya Juba na wapinzani kwani usalama na amani ya Sudan Kusini ni muhimu sana kwa Sudan.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na mpinzani wake mkubwa Riek Machar walifikia makubaliano ya amani mwaka 2018 ambapo kwa mujibu wa makubaliano hayo, pande hizo mbili hasimu zitagawana madaraka ya Sudan Kusini na kusimamisha mapigano kikamilifu baina yao. 

Sudan Kusini ilijitenga na Sudan tarehe 9 Julai 2011 na tangu mwaka 2013 hadi hivi sasa imetumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe na migogoro mingi ya ndani.

Tags

Maoni