Apr 06, 2020 13:22 UTC
  • Wapinzani wailaumu serikali ya Uganda kuhusu COVID-19; Waziri Mkuu wa zamani wa Libya afariki dunia kwa corona

Wapinzani nchini Uganda wameilaumu serikali ya Rais Yoweri Museveni kwa kushindwa kudhibiti maambukizi ya corona nchini humo kama ambavyo wamesisitiza kuwa chakula kinachotolewa na Serikali kuwasaidia waathirika wa corona hakitoshi.

Televisheni ya France 24 imeripoti habari hiyo na kumnukuu Waziri Mkuu wa Uganda, Bw. Ruhakana Rugunda akijibu malalamiko hayo ya wapinzani akisema, zoezi hilo la Serikali ni kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye shida zaidi tu si kwa ajili ya kila muathiriwa wa corona.

Zoezi la kugawa chakula ili kukabiliana na madhara ya kiuchumi na kijamii ya waathiriwa wa corona lilianza wiki mbili zilizopita nchini Uganda. Zoezi hilo linafanyika katika mji mkuu Kampala na maeneo mengine ya Uganda kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa corona. Hata hivyo wapinzani wanasema chakula kinachotolewa ni kidogo sana na hakikidhi haja.

Mahmoud Jibril

 

Wakati huo huo Waziri Mkuu wa zamani aliyeongoza serikali ya mpito nchini Libya, Mahmoud Jibril,  amefariki dunia kwa ugonjwa wa COVID-19 yaani corona.

Imeelezwa kuwa Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Libya aliyeongoza mapinduzi yaliyong'oa madarakani Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011 alilazwa katika hospitali moja mjini Cairo Misri baada ya kupata mshtuko wa moyo na siku tatu baadaye, aligundulika kuwa na ugonjwa wa COVID-19 na kuwekwa karantini. Mkurugenzi wa Hospitali ya Ganzouri iliyopo mjini Cairo, Hisham Wagdy, amesema Jibril alifikishwa hospitalini hapo Machi 21, 2020,  na alithibitishwa kuwa na corona siku chache baadaye.

Habari hiyo imethibitishwa pia na msaidizi wa Mahmoud Jabril katika chama chake yaani Fawzi Ammar ambaye amesema kuwa, Jibril amefariki dunia katika hospitali moja binafsi mjini Cairo Misri alikokuwa anatibiwa tangu mwezi uliopita.

Tags

Maoni