Apr 06, 2020 16:24 UTC
  • Uhuru Kenyatta
    Uhuru Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ametangaza hatua mpya zinazolenga kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19, ambao hadi sasa umewapata watu 158 na kuchukua roho za wagonjwa sita.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta Jumatatu ya leo ameamuru kusitishwa kwa harakati zote katika maeneo yote ya nchi yaliyoathiriwa zaidi na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na mji mkuu, Nairobi, katika hatua ya kukomesha maambukizi ya virusi vya corona.

Akihutubia taifa jioni ya leo, Kenyatta amesema amri hiyo inahusu maeneo ya jiji la Nairobi, sehemu ya Kaunti ya Kiambu hadi Chania River huko Thika, Rigori, Ndender, mji wa Kiambu, sehemu ya Kaunti ya Machakos hadi Athi River na maeneo ya Kaunti ya Kajiado.

Maeneo mengine ya Kenya ambako harakati zimepigwa marufuku ni pamoja na mji wa pwani wa Mombasa na Kaunti za Kilifi na Kwale.

Rais Kenyatta Amesema amri ya kuzuia harakati katika jiji la Nairobi itaanza kutekelezwa leo kwa kipindi cha siku 21.

Watu 6 wameaga dunia kutokana na virusi vya corona nchini Kenya

Amesisitiza kuwa virusi vya corona havina huruma, na kiwango cha kusambaa kwake, kama hakikudhibitiwa, kinakua kwa kasi kubwa.

Rais wa Kenya amesema idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona hadi hii leo nchini humo imefikia 158 baada ya watu wengine 16 kupatwa na virusi hivyo. Wagonjwa sita miongoni mwao wameaga dunia.

Na katika hatua za kupambana na corona, Rais wa Kenya ameiagiza Hazina ya Kitaifa kutumia Shilingi bilioni mbili zilizopatikana kutokana katika operesheni ya kupambana na rushwa na ufisadi kwa ajili ya kuwasaidia wahitaji, hasa katika maeneo ya mijini.

Wakati huo huo uchunguzi wa maoni unaonyesha kuwa watu saba kati ya kila Wakenya kumi wanamini kwamba serikali inapaswa kusitisha shughuli zote kikamilifu nchini.

Uchunguzi huo uliofanywa na shirika la utafiri na ushauri la Infotrak unaonyesha kuwa asilimia 75 ya Wakenya wana wasiwasi kuhusiana na virusi vya corona.

Tags

Maoni