Apr 07, 2020 14:29 UTC
  • Chad: Tumeshawatokomeza magaidi wote wa Boko Haram katika ardhi yetu

Serikali ya Chad imetangaza kuwa magaidi wote wa kundi la Boko Haram wameshatokomezwa na kutimuliwa katika ardhi ya nchi hiyo.

Msemaji wa serikali ya Chad Omar Yaya Hussein amesema leo kuwa, kufuatia operesheni ya mashambulio iliyopewa jina la "Operesheni ya Ghadhabu ya Bomo" iliyofanywa wiki iliyopita na jeshi dhidi ya ngome za Boko Haram, hakuna gaidi hata mmoja wa kundi hilo aliyesalia katika ardhi ya nchi hiyo.

Afisa huyo wa serikali ya Chad ameongeza kuwa, taarifa zaidi za matokeo ya operesheni hiyo dhidi ya kundi la kigaidi la Boko Haram yatatangazwa hivi karibuni.

Jeshi la Chad lilianzisha operesheni hiyo baada ya shambulio la Machi 31 lililofanywa Boko Haram katika eneo la Bomo lililoko kwenye mkoa la Ziwa Chad. Askari 98 waliuawa katika shambulio hilo ambalo lilitoa pigo kubwa zaidi kwa jeshi la Chad.

Magaidi wa kundi la Boko Haram

Japokuwa harakati za uasi na ugaidi wa kundi la Boko Haram zilianzia katika jimbo la Borno kaskazini mwa Nigeria mnamo mwaka 2009, lakini baadaye zilisambaa hadi nje ya mipaka ya nchi hiyo katika eneo la Ziwa Chad linalopakana na Nigeria yenyewe, Niger, Cameroon na Chad.

Boko Haram ni moja ya makundi ya kigaidi yanayosababisha maafa hasa ya roho za watu barani Afrika. Mengine ni kundi la Al-Shabaab la Somalia na Al-Qaeda katika eneo la Sahel.../

 

Tags

Maoni