Apr 07, 2020 14:59 UTC
  • Corona yamburuzisha mahakamani Naibu Gavana Kenya, mbunge Tanzania ataka waziri wa SMZ achukuliwe hatua

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema ni yeye aliyeamuru Naibu Gavana wa Kaunti ya Kilifi Gideon Saburi akamatwe kwa kile alichosema, uzembe aliofanya wa kukwepa karantini baada ya kurudi safarini kutoka nchini Ujerumani, hali ambayo iliweka hatarini maisha ya Wakenya dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona (COVID-19).

Akizungumza katika mahojiano aliyofanya leo na kituo kimoja che redio nchini Kenya, Kenyatta amesema, anaomba dua kiongozi huyo wa Kaunti ya Kilifi ahukumiwe kifungo cha miaka kumi jela kwa dharau aliyofanya kuhusiana na janga la COVID-19.

"Mimi ndiye niliyesema Naibu Gavana wa Kilifi akamatwe... Ninamuombea ahukumiwe kifungo cha miaka 10", amesema kiongozi huyo.

Rais wa Kenya amehoji: "Vipi kiongozi anasafiri kutoka Ujerumani na kuanza kuwaambukiza watu Nairobi na Kilifi?", na akaongeza kuwa nafasi ya madaraka aliyonayo haitamkinga na matokeo hasi ya vitendo vyake.

Rais Uhuru Kenyatta ametoa kauli hiyo siku moja baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka wa Serikali ya Kenya kutaka Saburi awekwe mahabusu katika jela yenye ulinzi mkali ya Manyani ili kuwezesha Polisi kukamilisha uchunguzi wao baada ya Naibu Gavana huyo kufikishwa mahakamani hapo jana.

Hayo yanajiri wakati nchini Tanzania malalamiko ya kutaka waziri anayedaiwa kuambukiza watu virusi vya corona achukuliwe hatua yalifika hadi kwenye bunge la nchi hiyo hapo jana. 

Waziri wa SMZ, Salama Aboud Talib

Mbunge wa jimbo la Konde kwa tiketi ya chama cha CUF Khatib Said Haji alimuomba Waziri Mkuu wa nchi hiyo Kassim Majaliwa amchukulie hatua stahiki Waziri wa Ardhi , Nyumba, Maji na Nishati wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Salama Aboud Talib, ambaye amesema, alikataa kukaa karantini na kusababisha maambukizi kwa watu wawili kwenye familia yake.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, waziri huyo alifanya hivyo kwa sababu ya kiburi cha madaraka yake. Akizungumza wakati wa kuhitimisha hotuba ya bajeti ya ofisi yake, Waziri Mkuu wa Tanzania alithibitisha taarifa kwamba, serikali ilimuondoa kwa nguvu katika hospitali ya Mnazimmoja, mjini Zanzibar na kumuweka karattini waziri huyo wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati SMZ na akaongeza kwamba, awali waziri huyo alikataa kukaa karantini.

Hadi sasa hakuna kauli rasmi iliyotolewa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wala hatua iliyotangazwa kuchukuliwa dhidi ya waziri huyo.../ 

Tags

Maoni