Apr 08, 2020 08:06 UTC
  • UN yataka kuachiwa haraka iwezekanavyo kiongozi wa upinzani wa Mali aliyetekwa nyara

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetaka kuachiwa huru haraka iwezekanavyo Soumaila Cisse kiongozi wa upinzani wa nchini Mali aliyetekwa nyara. Baraza hilo limezitolea wito serikali ya Mali na makundi yenye silaha ya nchi hiyo kuharakisha utekelezaji wa makubaliano ya amani ya mwaka 2015.

Cisse alitekwa nyara Machi 25 mwaka huu akiwa katika kampeni za uchaguzi katika wilaya ya Niafounke mkoani Timbuktu siku kadhaa kabla ya kufanyika uchaguzi wa bunge. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetaka kuachiwa huru kiongozi huyo wa upinzani nchini Mali kupitia taarifa yake iliyoitoa jana katika mkutano wake wa kwanza kufanyika kwa njia ya video katika kipindi cha karibu wiki nne kutokana na mlipuko wa maambukizi ya corona.  

Nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamelaani pia shambulio la kigaidi dhidi ya askari jeshi wa serikali ya Mali juzi Jumatatu huko Bamba katika mkoa wa Gao kaskazini mwa nchi hiyo ambapo wanajeshi wasiopungua 25 waliuliwa na sita kujeruhiwa.  

Itakumbukwa kuwa Mali imekuwa katika mivutano ya kisiasa tangu kuibuka machafuko nchini mwaka 2012 yaliyosababisha uasi wa baadhi ya wanajeshi na kumpindua Rais Amadou Toumani Toure ambaye aliiongoza nchi hiyo kwa muda kwa miaka 10. Hali hiyo ya mivutano ya kisiasa ilitoa mwanya kwa Ufaransa kuingilia kati kijeshi nchini humo na kuiondoa madarakani serikali hiyo ya kijeshi mwaka 2013.

Rais wa Mali aliyepinduliwa, Amadou Toumane Toure  

 

 

 

Tags

Maoni