Apr 09, 2020 13:10 UTC
  • Rais wa Botwana, Baraza la Mawaziri na wabunge wawekwa kwenye karantini kwa corona

Rais Mokgweetsi Masisi wa Botswana na Baraza lake zima la Mawaziri pamoja na wabunge wamewekwa kwenye karantini kuangaliwa iwapo wameambukizwa kirusi hatari cha corona au la.

Vyombo vya habari vimetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, uamuzi huo umefikiwa baada ya mfanyakazi mmoja wa masuala ya afya aliyekwenda kuwapima corona wabunge, kuthibitika kuwa yeye mwenyewe ameambukizwa ugonjwa wa COVID-19.

Zoezi la kuwapima mawaziri na wabunge lilifanyika jana Jumatano wakati walipokutana kujadili mwito wa Rais Mokgweetsi Masisi wa kuongezwa muda wa hali ya dharura nchini humo. 

Mkurugenzi wa afya ya umma wa Botswana, Malaki Tshipayagae, ametangaza habari hiyo leo Alkhamisi kwa njia ya televisheni ya taifa na kusema: Wabunge, mawaziri wote pamoja na rais watawekwa kwenye karantini kuanzia leo.

Bunge la Botswana

 

Mnaweza kukaa karantini majumbani mwenu kama mnataka, lau kama hilo haliwezekani tutakupatieni sehemu ya kukaa karantini, alisema Tshipayagae na kuongeza kuwa, tutakuwa tukikufanyieni uchunguzi kwa muda wa siku 14 zijazo na mkithibitika hamjaambukizwa corona, mtaondolewa kwenye karantini. 

Kesi za watu waliokumbwa na corona nchini Botswana imeongezeka mara mbili katika kipindi cha wiki moja. Hivi sasa wameshafikia watu 13. Rais Masisi ametoa mwito wa kutangazwa hali ya dharura kwa muda wa miezi sita nchini humo. Katiba ya Botswana inaruhusu siku 21 tu za muda wa dharura lakini muda huo unaweza kuongezwa kwa idhini ya Bunge. 

Tayari bunge la Botswana limepasisha pendekezo hilo la kutangazwa kipindi cha miezi sita ya dharura nchini humo kwa ajili ya kupambana na janga la kirusi cha corona.

Maoni