Apr 10, 2020 11:59 UTC
  • Benki ya Dunia: Afrika kuathirika kiuchumi kufuatia mlipuko wa virusi vya Corona

Benki ya Dunia imetangaza kuwa, uchumi katika mataifa mengi ya bara la Afrika, utayumba kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona mwaka huu wa 2020 kwa mara ya kwanza baada ya miaka 25.

Ripoti ya Benki hiyo inaeleza kwamba, ukuaji wa uchumi wa mataifa hayo utashuka kwa asilimia 2.1 na kufikia asilimia 5.1. Mwaka uliopita wa 2019, uchumi huo uliongezeka kwa asilimia 2.4.

Aidha, ripoti hiyo inaeleza kuwa, mataifa hayo yatapoteza kati ya dola bilioni 37 hadi bilioni 79 katika vita dhidi ya virusi hivyo ambavyo vimesabisha kukwama kwa shughuli za kawaida kama biashara na sekta ya utalii.

Benki ya Dunia na Shirika la Afya Duniani yanasema kuwa, yanajitahidi kutafuta fedha kuyasaidia mataifa ya Afrika kupambana na janga hili.

Wakati huo huo, ripoti mbalimbali zinaeleza kuwa, Marekani na Ulaya ambako kwa sasa ni kitovu cha virusi vya Corona hali ya uchumi itakuwa mbaya hata baada ya kumalizika kwa virusi vya Corona.

Takwimu za hivi karibuni kabisa kuhusiana na maambukizo ya virusi vya Corona zinaonyesha kuwa Marekani imeendelea kuongoza ikiwa na waathirika zaidi ya laki nne na nusu. Uhispania inashika nafasi ya pili ikiwa na waathirika zaidi ya laki moja na nusu wa virusi vya Corona. Italia ambayo inaongozwa kwa vifo vya Corona, inashika nafasi ya tatu kwa idadi ya maambukizi ya Corona.  Watu zaidi ya 18,000 wamefariki dunia hadi sasa nchini Italia kwa virusi vya Corona ikifuatiwa na Marekani ambapo watu karibu 17,000 wamepoteza maisha nchini humo huku kukiripotiwa uhaba mkubwa wa vifaa vya kukabiliana na virusi hivyo katika nchi hiyo.

Maoni