Apr 10, 2020 12:00 UTC
  • FAO: Tunaendeleza juhudi za kudhibiti nzige wa jangwani licha ya changamoto za Corona

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limetangaza kuwa, linaendelea na juhudi zake kwa kushirikiana na nchi athirika kwa ajili ya kudhibiti baa la nzige wa jangwani katika nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki licha ya kuweko vizingiti vya kusafiri watendaji wake na kusafirisha vifaa kutokana na mlipuko wa virusi vya Corona.

Taarifa ya FAO imeeleza kuwa takribani watu milioni 20 wanaathiriwa na uwepo wa nzige hao wanaoshambulia mazao katika nchi za Ethiopia, Kenya Somalia, Sudan Kusini na Uganda pamoja na watu wengine milioni 15 nchini Yemen ambako pia wadudu hao wamevamia.

Sehemu nyingine ya taarifa ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), imebainisha kwamba, mvua kubwa za mwezi uliopita zinatarajiwa kuchochea ongezeko la nzige hao katika eneo la Afrika Mashariki katika miezi ijayo huku wengine wakitatarajiwa kusafiri kutoka Kenya hadi Sudan Kusini na Uganda.

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO)

Maafisawa FAO wanasema kuwa, hadi sasa zaidi ekari 240,000 zimepuliziwa dawa ya kuua nzige katika eneo hilo la Afrika Mashariki na watu 740 wamepatiwa mafunzo ya kudhibiti nzige hao kutokea ardhini, lakini mlipuko wa virusi vya Corona umeleta changamoto katika upatikanaji wa mashine zenye mota za kupulizia dawa pamoja na dawa zenyewe za kuua wadudu.

Shirika hilo la FAO limesisitiza kuwa, hali ya mlipuko wa nzige wa jangwani bado ni mbaya katika nchi za Pembe ya Afrika na kwamba inahatarisha usalama wa chakula hususan katika nchi za Ethiopia, Uganda, Somalia na Kenya.

Baadhi ya ripoti zinaeleza kuwa, kwa sasa madhara ya nzige hao ni makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 25 iliyopita kwenye eneo la Afrika Mashariki na Asia Kusini.

Maoni