Apr 30, 2020 02:36 UTC
  • Msimamo wa Umoja wa Mataifa wa kukataa kuitambua serikali ya Libya aliyojitangazia Haftar

Kufuatia hatua ya Jenerali muasi Khalifa Haftar ya kukiuka mapatano ya Skhirat na kujitangazia serikali nchini Libya, Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa unaitambua rasmi tu Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa (GNA) yenye makao yake Tripoli.

Stephanie Williams, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya ametangaza kuunga mkono Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa Libya (GNA) inayoongozwa na Fayez al-Sarraj  na kuongeza kuwa: "Mabadiliko yoyote ya kisiasia nchini humo yanapaswa kufanyika kwa njia ya demokrasia.

Jenerali muasi Khalifa Haftar anayeongoza kundi la wanamgambo wanaojiita Jeshi la Taifa la Libya (LNA) siku ya Jumatatu alijitangaza mtawala mpya wa nchi hiyo katika hotuba aliyotoa kupitia televisheni na kuyafuta makubaliano ya mwaka 2015 yanayojulikana kama "Makubaliano ya Skhirat". Alisema ataongoza serikali ya mpito hadi wakati wa kufanyika uchaguzi.

Hatua hiyo ya Haftar imepelekea mgogoro wa Libya kuchukua sura mpya.

Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya imesema tangazo la Haftar ni mapinduzi ya serikali na ni njia ya kujaribu kufunika kushindwa kwake kijeshi. Katika wiki za hivi karibuni, wanamgambo wanaofungamana na Haftar wameshindwa vibaya katika mapigano na wanajeshi wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa Libya.

Aprili mwaka jana, Haftar alianzisha mapigano kwa lengo la  kuukalia kwa mabavu mji wa Tripoli na kuitimua serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya. Alianzisha mapigano wakati ambao mchakato mpya wa mazungumzo ya amani ya Libya ulikuwa nao pia ndio unaanza. Nukta hii inaashiria kuwa yeye na waitifaki wake hawakuwa wanataka mabadilishano ya madaraka kwa njia ya kisiasa.

Fayez al-Sarraj Waziri Mkuu wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa Libya (GNA)

Jenerali muasi Haftar anapata uungaji mkono wa nchi kama vile Saudi Arabia, Imarati (UAE), Misri na baadhi ya nchi za Ulaya na hivyo ni kwa idhini ya waungaji mkono hao ndio amevuruga mchakato wa kisiasa Libya. Wakati alipoanzisha hujuma dhidi ya Tripoli, Haftar alidhani kuwa angepata ushindi wa haraka na hivyo kuchukua madaraka lakini alikumbana na jibu kali la wanajeshi wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ambayo inapata uungaji mkono wa kijeshi wa Uturuki.

Pamoja na kuwa katika miezi michache iliyopita kumekuwa na jitihada za kutatua mgogoro wa Libya kupitia mazungumzo lakini jitihada hizo zimefeli na sasa mapigano nchini humo yameingia awamu mpya. Hivi sasa madola ya kigeni kama vile Imarati yameingia moja kwa moja katika medani ya vita nchini Libya kiasi kwamba ndege za kivita za Imarati zimedondosha mabomu katika maeneo kadhaa ya nchi hiyo.

Weledi wa mambo wanasema kuwa, Imarati inajaribu kumsaidia Haftar ili achukue udhibiti wa mji wa Tripoli na kwamba lengo kuu la Imarati ni kuzuia kuundwa serikali huru, yenye kujitegemea na thabiti nchini Libya. Ingawa Imarati inawaunga mkono wanamgambo wa Haftar lakini lengo lake kuu ni kuweza kudhibiti na kutumia vibaya utajiri mkubwa wa Libya.

Libya ni nchi muhimu na tajiri zaidi katika eneo la Afrika Kaskazini na inahesabiwa kuwa lango la kistratijia barani Afrika. Libya ina utajiri mkubwa wa mafuta na gesi pamoja na madini na pia kijiografia inapakana na Bahari ya Mediteranea na hali kadhalika iko karibu na mpaka wa bara la Ulaya. Kutokana na umuhimu huo, tokea alipopinduliwa na kuuawa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi mwaka 2011, nchi za eneo na nchi nyingi za Ulaya zimekuwa zikitekeleza sera za kuwa na satwa katika nchi hiyo na hivyo zimezuia kupatikana amani na uthabiti wa kisiasa nchini humo.

Mchakato wa kisiasa Libya umeonyesha wazi kuwa madola ya kigeni yanayowania kuwa na satwa katika nchi hiyo ni pamoja na  Marekani, Saudi Arabia, Imarati, Misri, Ufaransa na Uingereza katika upande mmoja na katika upande wa pili ni Uturuki, Qatar na Russia na baadhi ya nchi za Ulaya.  Nchi hizo zinaunga mkono pande zinazohasimiana kwa maslahi yao ya kisiasa na kiuchumi nchini Libya.

Jeneralia muasi Libya Khalifa Haftar anayepata himaya ya baadhi ya madola ya Magharibi na Kiarabu

Hivi sasa inalekea kuwa, Khalifa Haftar amepata idhini ya waungaji mkono wake kwa lengo la kuvuruga mchakato wa amani Libya na hivyo kauli yake ya kujitangazia serikali inakusudia kudunisha au kuhafifisha ushindi wa hivi karibuni wa kijeshi wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa. Hatua hiyo ya Haftar imepingwa vikali na jamii ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa.

Jaafar  Qanad Boshi, mtaalamu wa masuala ya Afrika Kaskazini anatathmini hali hiyo kwa kusema: "Kuendelea mchakato wa amani wa Skhirat bila shaka si kwa maslahi ya Haftar. Hii ni kwa sababu waungaji mkono wa Haftar, hasa Misri na Imarati, hawakutaka mchakato huu uendelee kwa sababu utapelekea kuundwa serikali ya kidemokrasia nchini Libya.

Kwa msingi huo Libya inakabiliana na mustakabali usiojulikana na wenye mgogoro mkubwa kutokana na uingiliaji wa madola ajinabi.

 

Tags

Maoni