May 04, 2020 06:22 UTC
  • Mwito wa UN wa kuanza tena mazungumzo ya amani Libya

Mapigano nchini Libya yanaendelea katika hali ambayo Umoja wa Mataifa kwa muda mrefu sasa umekuwa ukihimiza kukomeshwa mapigano na kuunganishwa nguvu katika kukabiliana na ugonjwa hatari wa corona katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika iliyoiathiriwa vibaya na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Hivi sasa Umoja wa Mataifa umeunda kamati maalumu ya kuzungumza na pande hasimu nchini Libya ili angalau zikubali kusimamisha mapigano. Katika taarifa yake, kamati hiyo imesema kuwa imezitaka pande hasimu nchini Libya zisimamishe vita kwa heshima ya mwezi mtukufu wa Ramadhani na kwa ajili ya kupambana kwa pamoja na ugonjwa  wa COVID-19 na pia zitumie fursa hiyo kuanzisha mazungumzo ya amani ya kutatua mgogoro wa nchi yao. Lakini pamoja na hayo, mapigano bado yanaendelea nchini humo.

Naam, mapigano makali yanaendelea katika maeneo tofauti ya Libya kati jeshi la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa inayotambuliwa kimataifa na wanamgambo wanaounda kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya chini ya jenerali muasi Khalifa Haftar. Tarehe 27 Aprili 2020, Khalifa Haftar alitangaza kuvunja makubaliano yaliyofikiwa tarehe 17 Disemba 2015 katika mji wa Skhirat, Morocco, ambayo ndiyo yaliyounda Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa. Hatua ya jenerali huyo muasi inaendelea kulaaniwa hadi leo hii.

Ahmed al Mismari, msemaji wa wanamgambo wa jenerali Khalifa Haftar amesema kuwa, tangazo la usimamishaji vita limetolewa na jamii ya kimataifa na nchi rafiki, lakini "Jeshi la Taifa la Libya" lina haki ya kujibu mashambulizi na kujihami kila linaposhambuliwa.

Juhudi kubwa za kupatanisha makundi hasimu Libya zinafanyika kimataifa, lakini makundi hayo hayaoneshi nia njema

 

Hata hivyo Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya imekataa kushiriki katika usimamishaji vita huo. Baraza la Uongozi la serikali hiyo limekataa usimamishaji vita uliotangazwa Khalifa Haftar kwa hoja kuwa hakuna dhamana yoyote katika madai ya kusimamisha vita ya jenerali huyo muasi. Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya inataka kuweko usimamishaji vita wenye dhamana ya kuheshimiwa na pande zote.

Serikali hiyo imesema, uvunjaji wa makubaliano uliofanywa na Khalifa Haftar huko nyuma umepoteza imani kabisa kwa jenerali huyo muasi na umethibitisha kuwa jenerali huyo anapenda kutenda jinai.

Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya imetoa ushahidi wa hoja zake hizo kwa kugusia makubaliano ya kusimamisha vita yaliyofikiwa kati ya pande mbili katika mazungumzo ya miezi michache iliyopita huko Moscow, Russia. Jenerali Khalifa Haftar hakuheshimu makubaliano hayo, hivyo kuanzia hapo Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya nayo ilitangaza kuwa haitotia tena saini mkataba wowote na jenerali huyo.

Saudi Arabia ni muungaji mkono mkubwa wa jenerali muasi Khalifa Haftar

 

Hali hiyo imezusha hofu kubwa kwa jamii ya kimataifa kiasi kwamba, Sven Jürgenson, balozi wa Estonia katika Umoja wa Mataifa ambaye nchi yake hivi sasa ndiye mwenyekiti wa Baraza la Usalama la umoja huo amesema: Matukio ya Libya yanatia wasiwasi mkubwa kwani inawezekana kufikia makubaliano ya kusimamisha vita lakini makubaliano hayo huvunjika mara moja na huo ndio uhakika ambao tumeuona kutoka kwa Haftar. 

Ukweli hi kuwa hivi sasa Libya iko katika hatari kubwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Kuna mikono mingi ya madola ajinabi katika matukio ya Libya. Kwa upande mmoja, nchi za Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Misri na baadhi ya nchi za Magharibi zinamuunga mkono kikamilifu jenerali muasi Khalifa Haftar na katika upande wa pili, Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa inaungwa mkono na mahasimu wa madola hayo ya Kiarabu kama vile Uturuki ambayo imetuma jeshi lake kwenda kuilinda Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa inayoongozwa na Waziri Mkuu, Fayez al Sarraj. Mbali ni mgogoro wa wahamiaji haramu, sasa hivi Libya ina mgogoro mpya wa ugonjwa wa corona, lakini kirusi kibaya zaidi kinachoitesa Libya kama ulivyosema Umoja wa Mataifa, ni pande hasimu hasa jenerali muasi Khalifa Haftar kutoheshimu hata kidogo ahadi zao, suala ambalo linavunja moyo juhudi za kweli za kutatua migogoro wa nchi hiyo.

Tags

Maoni