May 16, 2020 02:28 UTC
  • Senegal yalalamikia kitendo cha Ufaransa cha kuanzisha safari za ndege za upande mmoja kuingia Dakar

Rais Macky Sall wa Senegal amelaani kitendo cha shirika la ndege la Ufaransa kuanzisha safari za upande mmoja kuingia mjini Dakar, mji mkuu wa Senegal na kusisitiza kwamba, hadi sasa Ufaransa bado inazihesabu nchi za Afrika kuwa ni koloni lake.

Rais Sall ameyasema hayo katika kikao cha viongozi wa serikali ya nchi hiyo ambapo amelaani vikali hatua ya shirika la ndege la Ufaransa kutangaza kuanzisha safari zake za upande mmoja kuingia mjini Dakar kuanzia katikati ya mwezi Juni mwaka huu. Amesema kuwa kitendo cha shirika hilo kutoa tangazo lake kabla ya kufanya mazungumzo na viongozi wa Senegal, kinatokana na siasa za serikali ya Paris za kuitwisha matakwa yake nchi ya Senegal.

Rais Macky Sall wa Senegal

Ameongeza kwamba hatua hiyo inabainisha msimamo wa dharau ilionao Ufaransa ambao kwa mujibu wake serikali ya Paris inaendelea kuzihesabu nchi za Afrika kuwa bado ni koloni lake. Rais Macky Sall wa Senegal amezidi kubainisha kwamba, hadi sasa bado serikali yake haijachukua uamuzi kuhusiana na hatua hiyo ya  shirika la ndege la Ufaransa. Serikali ya Senegal ilizuia safari za kimataifa za ndege kuingia nchi hiyo hadi mwishoni mwa mwezi huu kwa shabaha ya kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona.

Tags