May 18, 2020 10:43 UTC
  • Jeshi la Libya lachukua udhibiti wa uwanja wa ndege za kijeshi kutoka wapiganaji wa Haftar

Jeshi la Libya leo Jumatatu limechukua udhibiti wa Uwanja wa Ndege za Kijeshi wa Al-Watiya kutoka kwa wapiganaji wa jenerali muasi Khalifa Haftar

Uwanja  huo wa ndege ulitekwa na wapiganaji wa Haftar miaka sita iliyopita. Ushindi huo umetangazwa na Idara ya Habari ya Oparesheni ya Kijeshi ya Burkan Al-Ghadab ambayo imekuwa ikiongoza mkakati wa kijeshi wa serikali ya Libya yenye makao yake Tripoli.

Mafanikio hayo yamekuja baada ya Jeshi la Libya kuharibu mfumo wa ulinzi wa anga wa Pantsir ambao  Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) iliwakabidhi wapiganaji wa Haftar masaa 48 yaliyopita.

Kituo cha Ndege za Kijeshi cha Al Watiya ni muhimu Libya na ni cha pili kwa umuhimu nchini humo baada ya kile cha uwanaj wa Mitiga. Kituo cha anga cha al-Watiyyah ni kituo cha kistratejia kwa vikosi vya Haftar magharibi mwa nchi hiyo; na vikosi hivyo vimekuwa vikiushambulia mji mkuu wa Libya, Tripoli kutokea kwenye kituo hicho.

Khalifa Haftar

Watu zaidi ya 1,500 wameuawa katika mji mkuu wa Libya, Tripoli, wengine wasiopungua 6,000 wamejeruhiwa na zaidi ya laki moja na nusu wamebaki bila makazi, tangu vikosi vinavyoongozwa na Haftar na kuungwa mkono na Misri, Saudi Arabia, Imarati pamoja na baadhi ya nchi za Magharibi vilipoanzisha hujuma na mashambulio mwezi Aprili mwaka jana kwa lengo la kuuteka mji mkuu huo wa Libya unaodhibitiwa na Serikali ya Muafaka wa Kitaifa inayotambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa.

Tags

Maoni