May 20, 2020 00:49 UTC
  • Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa nchini Libya: Sehemu inayomfaa Khalifa Haftar ni jela tu

Muhammad Al-Qiblawi, Msemaji wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya amesisitiza kwamba hakutakuwa na usuluhishi wowote pamoja na wapiganaji wa Khalifa Haftar wanaojiita 'Jeshi la Kitaiga la Libya' na kwamba jenerali huyo muasi hana mustakbali wowote nchini humo.

Sambamba na kubainisha suala hilo, Al-Qiblawi amesema kuwa, sehemu anayofaa kuwa Haftar ni jela tu. Ameongeza kwamba Fayez al-Sarraj, Mkuu wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa nchini Libya ameshaweka wazi kwamba Khalifa Haftar hana nafasi yoyote kwenye mwenendo wa kisiasa na kamwe hatofanya naye mazungumzo. Msemaji wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya pia ameongeza kuwa serikali yake itaishitaki Imarati katika mahakama za kimataifa kutokana na hatua zake za kuingilia masuala ya ndani ya Libya na uungaji mkono wake kwa wapiganaji wa Jenerali Haftar. 

Muhammad Al-Qiblawi, Msemaji wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya

Muhammad Al-Qiblawi amefafanua kwamba ni suala lisilo na shaka kwamba serikali ya Imarati ni mshirika katika kumwaga damu ya watu wa Libya. Jumatatu Fayez al-Sarraj, Mkuu wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa alitangaza habari ya kukombolewa kambi ya kijeshi ya Al Watiya kutoka kwa wanamgambo wa Khalifa Haftar. Kambi hiyo ya kijeshi ina ghala la silaha, kituo cha mafuta, ngome na uwanja wa ndege za kivita. Hii ni katika hali ambayo Haftar amedai kwamba wapiganaji wake wameondoka kwenye kambi hiyo muhimu kama mojawapo ya mbinu za kivita.

Tags

Maoni