May 20, 2020 07:56 UTC
  • Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa Libya: Imarati inakiuka sheria za kimataifa

Mwakilishi wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya (GNA) katika Umoja wa Mataifa amesema: Umoja wa Falme za Kiarabu unakiuka sheria za kimataifa kwa kutuma silaha nchini Libya.

Taher Al-Sunni, mwakilishi wa GNA katika Umoja wa Mataifa ametoa kauli hiyo katika kikao cha Baraza la Usalama la umoja huo kilichofanyika kwa njia ya video kwa lengo la kuchunguza matukio ya Libya na akaeleza kwamba, ana hoja madhubuti na ushahidi kadhaa unaoonyesha kuwa Imarati imekiuka azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kuwasaidia na kuwaunga mkono waasi nchini Libya na kuwapelekea silaha na zana za kijeshi.

Fayez al-Sarraj (kulia) na Khalifa Haftar

Al-Sunni ameongeza kuwa, vikosi vya serikali ya mwafaka wa kitaifa ya Libya zimekuta silaha katika maeneo yaliyokuwa yakidhibitiwa na kundi la Khalifa Haftar ambazo nyingi zao ni za Imarati.

Mwakilishi wa kudumu wa Libya katika Umoja wa Mataifa ametilia mkazo umuhimu wa kutekelezwa azimio 2292 la Baraza la Usalama linalopiga marufuku uuzaji na utumaji silaha nchini Libya na akaongeza kwamba, endapo zitataka kupelekwa silaha nchini humo, suala hilo lifanyike kwa uelewa na kuafikiwa na serikali ya mwafaka wa kitaifa ya nchi hiyo.

Inasemekana kuwa, katika ripoti ya siri iliyowasilishwa hivi karibuni kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imeelezwa kwamba: Imarati inashiriki katika kusimamia njia ya siri ya anga kwa ajili ya kupeleka silaha huko Libya ili kulisaidia na kuliunga mkono kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya (LNA) linaloongozwa na Khalifa Haftar; na kwamba hatua hiyo inakiuka azimio linalopiga marufuku uingizaji silaha nchini humo.../

 

Tags

Maoni