May 21, 2020 10:45 UTC
  • Mufti wa Libya: UAE inawaua watu wa Libya

Mufti wa Libya amelaani vikali uingiliaji wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) katika masuala ya ndani ya nchi yake na kusema, "UAE inawaua watu wa Libya."

Kwa mujibu wa tovuti ya Arabi21, Sheikh Sadiq Al-Ghariani ametuma ujumbe ambapo ameashiria hatua ya UAE ya kuwapa silaha wapiganaji wa jenerali muasi Khalifa Haftar na kusema: "Ndege zisizo na rubani za UAE zinamwaga damu na kuua watu wa Libya."

Al-Ghariani aidha ametoa shukrani zake za dhati kwa serikali za Qatar na Uturuki kutokana na msaada wao kwa watu wa Libya.

UAE ni muungaji mkono mkuu wa wanagambo wanaojiita  'Jeshi la Kitaifa la Libya' ambao wanaongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar.

Wanamgambo hao ambao wanakalia eneo la mashariki mwa Libya pia wanapata msaada wa Misri na Saudi Arabia na baadhi ya nchi za Magharibi na hivi karibuni wameanza kuekelea maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo. 

Watu zaidi ya 1,500 wameuawa katika mji mkuu wa Libya, Tripoli, wengine wasiopungua 6,000 wamejeruhiwa na zaidi ya laki moja na nusu wamebaki bila makazi, tangu vikosi vinavyoongozwa na Haftar vianzishe hujuma na mashambulio mwezi Aprili mwaka jana kwa lengo la kuuteka mji mkuu huo wa Libya unaodhibitiwa na Serikali ya Muafaka wa Kitaifa inayotambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa.

Jenerali muasi Khalifa Haftar.

Ni vyema kuashiria kuwa, Libya ina serikali mbili hasimu, moja ikiwa na makao yake mjini Tobruk, iliyoko karibu na Jenerali Haftar, na nyingine ya Serikali ya Mapatano ya Kitaifa Libya inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Libya ilitumbukia katika machafuko na vita vya ndani baada ya wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wale wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.

Maoni