May 21, 2020 10:59 UTC
  • UN yapongeza nchi za Afrika kutokana na hatua  imara za kukabiliana na COVID-19

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezipongeza nchi za Afrika kutokana na jinsi zilivyochukua hatua haraka kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19 au corona akisema kuwa ingawa idadi ya vifo hivi sasa ni ndogo kuliko ilivyodhaniwa, bado kuna mambo mengi yamesalia.

Katika taarifa, Guterres amesema janga la COVID-19 linatishia maendeleo ya Afrika na kwamba litaongeza ukosefu wa usawa uliokuwa umedumu na pia njaa, utapiamlo na hatari ya kupata magonjwa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema tayari, mauzo ya bidhaa kutoka Afrika, utalii na utumaji fedha barani humo vinapungua na kwamba mamilioni wako hatarini kutumbukia kwenye umaskini.

Guterres amesema Umoja wa Mataifa unaonesha mshikamano kwenye vita dhidi ya COVID-19 kwa kusambaza mamilioni ya vikasha vya uchunguzi wa virusi, mashine za kusaidia wagonjwa kupumua na vifaa vingine kwenye maeneo mbali mbali barani Afrika.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa mapendekezo ambayo yataziwezesha nchi za Afrika kukabiliana na janga la COVID-19. Guterres ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za kimataifa kuimarisha mifumo ya afya barani Afrika, kuendeleza usambazaji wa chakula, kuepuka janga la kifedha, kusaidia elimu, kulinda ajira, kuwezesha biashara kujimudu, kusaidia mapato yaliyopotea yakiwemo ya mauzo ya bidhaa nje ya nchi.

Hadi kufikia leo Mei 21, idadi ya walioambukizwa COVID-19 barani Afrika ilikuwa watu 95,482  na miongoni mwao wasiopungua 3,000 wamefariki na wengine 38,120 wamepona.

 

Tags

Maoni