May 22, 2020 08:07 UTC
  • Chama cha Republican cha Tunisia: Umoja na muqawama, njia pekee ya kuikomboa Palestina

Katibu Mkuu wa chama cha Republican cha Tunisia amesema utawala ghasibu wa Israel hauelewi lugha nyingine isipokuwa ya mapambano na kusisitiza kuwa, "umoja na muqawama ndiyo njia pekee ya kuikomboa Palestina."

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Essam al-Shaabi akisema hayo kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds inayoadhimishwa hii leo katika pembe mbalimbali za dunia.

Ameashiria himaya na uungaji mkono wa Rais Donald Trump wa Marekani kwa Wazayuni na kueleza bayana kuwa, dunia inapaswa kuisusia na kuitenga Washington kwa kuwanga mkono Wazayuni.

Katibu Mkuu wa chama cha Republican cha Tunisia amesema serikali na mataifa ya dunia yana wajibu wa kutetea haki za Wapalestina kwa kuunga mkono mhimili wa muqawama na misingi ya kadhia ya Palestina.

Siku ya Quds ya mwaka huu kwa sehemu kubwa inaadhimishwa mitandaoni kutokana na janga la corona

Kadhalika mwanasiasa huyo wa Tunisia amesema lengo la Imam Khomeini (MA), Muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuainisha Ijumaa ya mwisho ya mwezi wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds, ni kuwapa jukwaa Waislamu na wapenda haki kote duniani kuonyesha ghadhabu na chuki zao kwa sera za kibaguzi za utawala haramu wa Israel.

Tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979, Siku ya Kimataifa ya Quds imekuwa ikiadhimishwa kupitia maandamano na makongamano kote duniani.

 

Tags

Maoni