May 23, 2020 10:42 UTC
  • Baadhi ya Waislamu katika nchi za Mashariki na Magharibi mwa Afrika wasali Iddi leo

Baadhi ya Waislamu katika nchi kadhaa za mashariki na magharibi mwa Afrika wamesali na kusherehekea sikukuu ya Idul-Fitr, huku aghalabu ya Waislamu duniani wakitazamiwa kuadhimisha sala na sherehe hizo kesho Jumapili.

Waziri wa Masuala ya Dini wa Somalia, Sheikh Nur Mohamed Hassan jana usiku alitangaza kwamba mwezi umeonekana viungani mwa mji mkuu Mogadishu, na hivyo hii leo taifa hilo la Pembe ya Afrika limesali Sala ya Iddul-Fitr.

Aidha Rais Mohamed Abdullahi Farmaajo wa nchi hiyo amewapongeza wananchi wa Somalia kwa kumaliza funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani huku akiwapa mkono wa kheri na fanaka wanaposherekea Iddul-Fitr.

Duru za habari zinaarifu kuwa, baadhi ya Waislamu pia wamesali na kuadhimisha sikukuu ya Iddul-Fitr katika nchi za Kenya, Tanzania na Ethiopia.

Aghalabu ya nchi duniani zinatamiwa kuadhimisha sikukuu ya Iddul-Fitr kesho Jumapili

Kadhalika baadhi ya Waislamu katika nchi za magharibi mwa Afrika za Senegal, Gambia na Mali wamesali Sala ya Iddi hii leo. Hata hivyo kiongozi wa Waislamu Nigeria, Sultan wa Sokoto ametangaza kuwa leo wamekamilisha funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani na kwamba Sala ya Iddi itasaliwa kesho Jumapil. Amesema amefikia uamuzi huo kwa kutoshuhudiwa mwezi mwandamo.

Baadhi ya wanajimu wanasema ilikuwa muhali kushuhudia mwezi mwandamo jana magharibi katika sehemu yoyote ile duniani, kwa kuwa mwezi wenyewe ulizaliwa jana.

 

 

Tags

Maoni