May 23, 2020 15:44 UTC
  • Waziri wa Afya wa Tanzania: Mashine moja ya kupima Corona ilikuwa na matatizo

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Tanzania Ummy Mwalimu ametoa taarifa kuhusu uchunguzi uliofanywa kuilenga maabara ya taifa ambapo ameeleza mambo kadhaa yaliyogunduliwa na kamati teule ya uchunguzi huo.

Kwa mujibu wa Waziri Ummy, kamati imegundua uwepo wa mapungufu kadhaa katika mfumo wa kimuundo, kiutendaji na uendeshaji wa kitaaluma katika upimaji wa vipimo, uhakiki wa ubora wa majibu na udhaifu katika uhifadhi wa vipimo vya ugonjwa wa Covid-19. Ameendelea kufafanua kuwa, moja ya mashine za kupima sampuli za virusi vya Corona ilikua na hitilafu bila huku uongozi wa maabara ukishindwa kuchukua hatua za kuifanyia matengenezo mashine hiyo kwa wakati. “Upimaji wa Sampuli zote za Covid-19 umehamishiwa katika maabara mpya iliyokamilika kujengwa katika eneo la Mabibo Dar es Salaam ambayo kwa sasa ndiyo itakuwa maabara ya Ttaifa ya afya ya jamii." Amesema Waziri wa Afya wa Tanzania. Aidha amesema kwamba mabara hiyo mpya ina uwezo wa kupima sampuli 1800 za ugonjwa wa Covid -19 ndani ya masaa 24 tofauti na ile ya awali iliyokua na uwezo wa kupima sampuli 300 pekee. “Mojawapo ya Mashine za kupima sampuli za Covid-19 ilikua na hitilafu bila uongozi wa maabara kuchukua hatua za kuifanyia matengenezo kwa wakati.” Amesema Ummy Mwalimu.

Isack Kamwelwe, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Katika hatua nyingine Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema kuwa ndege ya kwanza iliyobeba watalii kutokea Ugiriki ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) hapo  jana. Akizungumza jana na waandishi wa habari Kamwelwe alisema ndege iliyobeba watu saba wakiwemo watalii wanne kutoka Ugiriki, ilitua jana asubuhi, ikiwa ni siku chache baada ya serikali kutangaza kufungua anga lake, lililokuwa limefungwa kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona. “Ndege iliyotua ilikuwa na watalii wanne na crew ya watu watatu na wametua tayari wamepokelewa na wameenda kuangalia wanyama.” Alisema. Aidha alisema kuwa tayari kuna ratiba ya ndege, zitakazofanya safari zake kwenda Tanzania na nafasi zimejaa, huku akisisitiza kwamba ifikapo tarehe 28 Mei mwaka huu ndege nyingi zitatua nchi hiyo.

 

 

 

Tags

Maoni