May 24, 2020 11:20 UTC
  • Jeshi la Nigeria laangamiza makumi ya magaidi kaskazini mwa nchi

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Nigeria amesema wanajeshi wa nchi hiyo wamefanikiwa kuua wanachama 135 wa magenge ya kigaidi katika majimbo ya Zamfara na Katsina kaskazini magharibi mwa nchi.

Shirika la habari la Xinhua limemnukuu John Enenche akisema hayo katika taarifa ya jana Jumamosi na kuongeza kuwa, magaidi hao wameuawa katika operesheni iliyopewa jina la 'Hadarin Daji' iliyofanyika baina ya Jumatano na Ijumaa iliyopita.

Amesema jeshi hilo limetekeleza mashambulizi ya anga dhidi ya ngome za magenge hayo ya kigaidi yanayoonekana kuanza kujikusanya upya katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Hata hivyo hajaeleza iwapo magaidi hao waliouawa katika operesheni hiyo ya siku tatu wana mfungamano wowote na genge la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram au la.

Wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya askari saba wa jeshi la Nigeria kuuawa katika mashambulizi mawili tofauti ya kundi la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram kaskazini mashariki mwa nchi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, wanajeshi hao waliuawa baada ya wananchama wa genge hilo kushambulia mji wa Dapchi na kijiji cha Maza, kaskazini mashariki mwa Nigeria. 

Tags

Maoni