May 25, 2020 03:56 UTC
  • Sudan yakaribia

Katika hatua nyingine ya kushangaza na ambayo inaashiria jinsi Israel ilivyo na hamu ya kuimeza nchi ya Waislamu ya Sudan, Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni amezungumza kwa simu na mkuu wa Baraza la Uongozi la Sudan na kuitaka Khartoum ijikurubishe zaidi na zaidi kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Shirika la habari la FARS limenukuu taarifa iliyotangazwa na ofisi ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni ambayo imesema, Netanyahu amefanya mazungumzo ya simu na Abdul Fattah al Burhan, mkuu wa Baraza la Uongozi la Sudan na kutaka uhusiano wa pande mbili uimarishwe kwenye nyuga zote kwa kadiri inavyowezekana.

Itakumbukwa kuwa mkuu huyo wa Baraza la Uongozi la Sudan, mwezi Februari mwaka huu alizusha kelele nyingi baada ya kutoka Sudan na kwenda kuonana na Benjamin Netanyahu nchini Uganda. Hadi leo moto wa kulaaniwa al Burhani kwa uhalifu na usatili wake huo bado haujazima. 

Baadhi ya mawakili wamefungua kesi mahakamani kumshitaki Abdul Fattah al Burhan kwa kufanya jinai na usaliti huo wa kuonana na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu. 

Ujumbe wa Facebook wa ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel kuhusu mazungumzo ya simu ya Netanyahu na Burhan

 

Chama cha Congress ya Wananchi cha Sudan nacho kililaani vikali na kilisema katika tamko lake kwamba al Burhan amelivunjia heshima taifa la Sudan kwa kukutana kwake na Benjamin Netanyahu. 

Katika miezi ya hivi karibuni, utawala wa Kizayuni wa Israel umeongeza njama za kujenga uhusiano mzuri zaidi na nchi za Afrika. 

Nchi za Afrika zina akiba na utajiri mkubwa wa mafuta na madini hasa almasi na urani na ndio maana Wazayuni wanatafuta kila njia kuhakikisha wanapora zaidi na zaidi utajiri huo mkubwa wa maliasili wa bara la Afrika.

Tags

Maoni