May 25, 2020 03:57 UTC
  • Arab League: Mgogoro wa Libya hauwezi kutatuliwa kijeshi

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) ametaka kusimamishwa mara moja mapigano nchini Libya na kuanza mazungumzo ya kisiasa haraka iwezekanavyo chini ya usimamiaji wa Umoja wa Mataifa akisisitiza kuwa utatuzi wa mgogoro wa nchi hiyo ni wa kisiasa si wa kijeshi.

Hayo yameripotiwa na televisheni ya Sky News ambayo imemnukuu Ahmed Aboul Gheit, Katibu Mkuu wa Arab League akisema jana Jumapili katika ujumbe wake wa Idul Fitr kwamba, mgogoro wa Libya hautoweza kutatuliwa bila ya kukomeshwa kwanza uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Aidha amesisitiza kuwa, mgogoro wa Libya kamwe hauwezi kutatuliwa kwa njia za kijeshi na amewataka viongozi wa nchi hiyo kuitikia mwito wa kimataifa wa kuacha mapigano na kuanzisha mara moja mazungumzo ya kisiasa ya kutatua mgogoro wa nchi yao.

Jenerali muasi Khalifa Haftar katika mazungumzo na mfalme wa Saudi Arabia, Salman bin Abdulaziz

 

Kundi linalojiita "Jeshi la Taifa la Libya" linaloongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar ambaye kwa miaka mingi anaungwa mkono na Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Misri na baadhi ya nchi za Magharibi, hivi sasa anadhibiti eneo la mashariki mwa Libya.

Mwezi Aprili mwaka jana wakati juhudi za kuutatua kisiasa mgogoro wa Libya zilipokuwa zimekaribia kuzaa matunda, jenerali huyo muasi alianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya mji mkuu Tripoli kwa baraka kamili za nchi zinazomuunga mkono kwa tamaa ya kuiteka haraka Tripoli. Hata hivyo ndoto yake hiyo imeshindwa kutimia kutokana na muqawama wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa iliyoundwa na Umoja wa Mataifa.

Maoni