May 25, 2020 04:37 UTC
  • Watu 25 wauawa na kujeruhiwa katika mripuko wa bomu kusini mwa Somalia

Duru za habari nchini Somalia zimeripoti kujiri mripuko wa bomu Jumapili usiku katika mji wa Baidoa, kusini mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti, bomu hilo liliripuka wakati wa sherehe za Idul-Fitr katika mji huo. Aidha duru za habari zimearifu kwamba katika hujuma hiyo kwa akali watu watano wameuawa na wengine 20 wamejeruhiwa. Hadi sasa hakuna kundi lililotangaza kuhusika na shambulizi hilo, ingawa inadhaniwa kwamba kundi la kigaidi la ash-Shabab ndilo lililotekeleza jinai hiyo. Kundi la ash-Shabab lenye mfungamano na kundi la kigaidi la Al-Qaidah hadi sasa limehusika na utegaji mabomu na mashambulizi mengi ndani ya Somalia na katika nchi jirani.

Wanachama wa kundi la kigaidi la ash-Shabab nchini Somalia

Aidha kundi hilo limekuwa likifanya juhudi za kuiondoa madarakani serikali ya Somalia kuanzia mwaka 2007. Hata hivyo mwaka 2011 kundi hilo lilitimuliwa kutoka mjini Mogadishu na jeshi la serikali kwa kushirikiana na askari wa Umoja wa Afrika AMISOM. Pamoja na hayo, bado limeendelea kudhibiti maeneo mengi ya vijijini nchini Somalia. Nchi hiyo ni moja ya nchi masikini zaidi na isiyo na uthabiti duniani.

Maoni