May 25, 2020 12:13 UTC
  • Ethiopia yagundua wagonjwa wapya 88, idadi yafikia 582

Ethiopia imethibitisha kugunduliwa wagonjwa wengine 88 wa COVID-19 na kufanya idadi ya kesi za corona zilizogunduliwa nchini humo hadi leo Jumatatu asubuhi kufikia 582. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa jana na Wizara ya Afya ya Ethiopia.

Hii ni idadi kubwa zaidi kuwahi kugunduliwa kwa siku moja katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika ambapo juzi Jumamosi ilitangaza kugundua wagonjwa 61 wa COVID-19.

Wizara ya Afya ya Ethioopia imesema, wagonjwa wote 88 wa corona waliothibitishwa jana Jumapili ni raia wa Ethiopia. 51 kati yao ni wanaume na 37 ni wanawake na umri wao ni baina ya miaka minane hadi 75.

Wizara hiyo aidha imesisitiza kuwa, kati ya wagonjwa hao 88 wa COVID-19, 13 wamewahi kusafiri nje ya Ethiopia, 20 walikuwa na mawasiliano na wagonjwa wa corona wanaojulikana na 55 waliobakia hawajawahi kusafiri nje ya Ethiopia na wala hawajawahi kuwa na mawasiliano na wagonjwa wanaojulikana wa corona.

Siku ya Jumapili, Mei 24, 2020 Ethiopia iligundua wagonjwa wapya 88 wa corona

 

Wizara ya Afya ya Shirikisho la Ethiopia pia imesema, hadi hivi sasa wagonjwa 152 wa COVID-19 wamepona na kuruhusiwa kurejea nyumbani. Huko nyuma wizara hiyo iliwahi kuthibitisha kuwa watu watano wamefariki dunia kwa corona nchini humo. 

Ethiopia ni nchi ya pili yenye watu wengi barani Afrika. Ina watu milioni 107. Kesi ya kwanza ya corona ilithibitishwa tarehe 13 Machi mwaka huu nchini humo.

Serikali ya Ethiopia imeweka sheria nyingi na kali za kupambana na maambukizi ya corona hasa kwa vile nchi hiyo ni Makao Makuu ya Umoja wa Afrika na inapokea wageni wengi.

Tags

Maoni