May 25, 2020 12:13 UTC
  • Kiongozi mmoja wa ISIS atiwa mbaroni nchini Libya

Kundi linalojiita "Jeshi la Taifa la Libya" limedai kumtia mbaroni kiongozi mmoja wa genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) nchini humo.

Televisheni ya Sky News imemnukuu Ahmed al Mismari, msemaji wa wanamgambo wa Jenerali Khalifa Haftar wanaojiita "Jeshi la Taifa la Libya" akisema hayo na kuongeza kuwa, kiongozi huyo wa magaidi wa Daesh ametiwa mbaroni katika viunga vya Tripoli, mji mkuu wa Libya.

Amesema, gaidi huo anayejiita Mohammed al Rawidhani, ni mmoja wa magaidi hatari na wakubwa sana wa ISIS aliyefanya jinai kubwa nchini Syria na ametiwa mbaroni katika viunga vya Tripoli hata hivyo hakusema ni lini tukio hilo limetokea.

Msemaji huyo wa "Jeshi la Taifa la Libya" pia amesema, gaidi huyo amepelekwa nchini Libya na mashirika ya kijasusi ya Uturuki.

Ujerumani nayo inashutumiwa kwa kutuma silaha Libya licha ya marufuku ya UN

 

Uturuki inashutumiwa kwa kutuma nchini Libya magaidi waliofanya jinai kubwa dhidi ya wananchi na maafisa wa serikali ya Syria.

Uturuki inadai kuwa inaisaidia Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa iliyoundwa na Umoja wa Mataifa chini ya Waziri Mkuu, Fayes al Sarraj.

Mwaka jana, al Sarraj alikutana na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki mjini Ankara na baada ya hapo Uturuki ilituma wanajeshi wake nchini Libya kuisaidia Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa.

Kwa upande wake, wanamgambo wa "Jeshi la Taifa la Libya" wanaungwa mkono na mahasimu wakubwa wa Uturuki yaani Saudi Arabia, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na baadhi ya nchi za Magharibi.

Waungaji mkono wa wanamgambo hao wametoa tamko la pamoja kuilaani Uturuki kutuma wanajeshi wake huko Libya.

Tags

Maoni