May 26, 2020 07:16 UTC
  • Mpango wa siri wa operesheni ya nchi kadhaa za Magharibi dhidi ya Libya wafichuliwa

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamefichua mpango wa siri wa nchi kadhaa za Magharibi ikiwemo Marekani na Uingereza katika kuwaunga mkono wapiganaji wa jenerali muasi Khalifa Haftar nchini Libya.

Ripoti za siri za Umoja wa Mataifa zinaarifu kwamba kwa akali watu 20 kutoka Australia, Ufaransa, Malta, Afrika Kusini, Uingereza na Marekani wanashiriki katika mradi uliopewa jina la 'OPUS' wa kumuunga mkono Jenerali Khalifa Haftar, anayedhibiti eneo la mashariki mwa Libya. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu hao walisafiri mwezi Juni mwaka jana kuelekea Libya kutokea Amman, mji mkuu wa Jordan na ndege ya mizigo kwa ajili ya kazi rasmi iliyotajwa chini ya anuani ya safari kutoka jumuiya ya kielimu kwa lengo la kufanya uchunguzi kuhusu matukio ya Libya.

Operesheni hiyo ilitumwa kwa lengo la kuzuia uungaji mkono wa Uturuki kwa serikali ya Fayez al-Sarraj

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyofichuliwa na Umoja wa Mataifa, ujumbe huo kimsingi ulitumwa kwenda kumuunga mkono Khalifa Haftar huku jukumu kuu la kundi hilo ambalo watu wake walitoka katika mashirika ya kijeshi ya nchi zilizotajwa ikiwa ni kuzuia harakati za meli za Uturuki zinazoelekea pwani ya Tripoli. Shirika la Habari la Ujerumani limeripoti kwamba Umoja wa Mataifa umetoa ripoti kuwa, upangaji ratiba wa operesheni hiyo ulisimamiwa na mashirika yenye makao yake nchini Imarati, ambapo hata hivyo ilivunjwa kutokana na sababu zisizojulikana. Mwaka jana Uturuki na serikali ya mwafaka wa kitaifa nchini Libya inayoongozwa na Fayez al-Sarraj zilitiliana saini mikataba miwili muhimu kuhusiana na mipaka ya bahari ya Libya na Uturuki katika maji ya Mediterania na pia kuhusu kupanuliwa ushirikiano wa kiusalama na kijeshi kati ya pande mbili. Mkabala wake nchi za Misri, Imarati, Saudi Arabia, Ufaransa, Cyprus na Ugiriki zinaiunga mkono serikali ya mashariki mwa Libya inayoongozwa na jenerali muasi, Khalifa Haftar.

Tags

Maoni